Mawaziri wa Kundi la Nchi zilizoendelea kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi wameazimia kuwa na Msimamo wa Pamoja katika Masuala Muhimu yatakayojadiliwa katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Mkutano huo ulioanza Septemba 28 hadi 29, 2023 jijini Dakar, Senegal umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Mhe. Dkt. Selemani Jafo.
Akizungumzia mkutano huo, Waziri Jafo amesema yaliyojadiliwa ni tathmini ya kidunia kuhusu utekelezaji wa Makubaliano ya Paris unaosisitiza haja ya kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuepuka kuongezeka kwa athari na kiwango cha ongezeko la wastani la joto duniani kuvuka nyuzi joto 1.5.
Pamoja na kiwango cha fedha za mabadiliko ya tabianchi kuongezeka imebainishwa bado ni kidogo na hakikidhi mahitaji hivyo, iliazimiwa kuwa matokeo ya tathmini hiyo yawe chachu ya upatikanaji wa fedha hizo.
Aidha, Dkt. Jafo amesema kuwa mkutano ulibainisha kuwa ahadi ya nchi zilizoendelea ya ukusanyanyaji wa Dola za Marekani Bilioni 100 ifikapo mwaka 2025 haijatimizwa, hivyo uhaba wa fedha ni changamoto kwa nchi zinazoendelea na hazikidhi mahitaji ya kukabiliana na changamoto zilizopo.
Kutokana na hali hiyo iliazimiwa kuwa taratibu za upatakanaji wa fedha kutoka katika Mifuko ya Mabadiliko ya Tabianchi zirahisishwe, kutimizwa kwa ahadi ya nchi zilizoendelea ya ukusanyaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kuongeza kiwango cha fedha kukidhi mahitaji.
Dkt. Jafo amesema kuwa majadiliano hayo pia yalijikita kuhusu muundo wa Mfuko wa Kushughulikia Hasara na Uharibifu Utokanao na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, taasisi itakayosimamia Mfuko, vyanzo vya fedha na utaratibu wa upatikanaji wa fedha kwa nchi zitakazokidhi vigezo.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Mfuko huo haujaanza kufanya kazi hivyo, msisitizo ulitolewa uanze kufanya kazi haraka iwezekanavyo kutokana madhara na hasara kubwa za athari za mabadiliko ya tabianchi hasa kwa nchi zinazoendelea.
“Nchi zimeweka msisitizo kuwa Mfuko upatiwe fedha haraka iwezekanayo kwa na hata nchi zote zinazoendelea kuwa na sifa na kustahili kutumia Mfuko huo na pia kuwe na utaratibu rahisi wa upatikanaji wa fedha kutoka kwenye Mfuko, Fedha zinazotolewa ziwe msaada na si mkopo na pia kutoathiri kiwango cha fedha za kuhimili mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unatarajiwa kufanyika Novemba 30 hadi 12 Disemba, 2023 Dubai, Falme za Nchi za Kiarabu (UAE).