Imeelezwa kuwa Ushirikiano uliopo baina ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kiasi kikubwa utasaidia kutoa haki kwa Wananchi na kutoa huduma bora.
Hayo yameelezwa leo Septemba 29, 2023 Jijini Dodoma na Viongozi mbalimbali katika ufunguzi wa Kikao cha Menejimenti ya ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Akifungua Kikao hicho Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Silvester Mwakitalu amesema umoja uliopo katika kufanya kazi kwa Taasisi hizo ni salamu tosha kwa wahalifu kuacha kufanya uhalifu kwa kuwa wapo makini kuhakikisha hakuna uhalifu unaotokea bila ya kuchukuliwa kwa hatua.
DPP Mwakitalu alisema kuwepo kwa uhalifu ukiwemo wa Vitendo vya Rushwa, uhujumu uchumi na dawa za kulevya kunarudisha nyuma maendeleo ya Taifa.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Hamdun alisema kuwepo kwa kikao hicho kila mwaka kunatoa fursa ya kujitahmini na kubaini mapungufu ya kiutendaji na hatimaye kuweka mikakati ya kuboresha ili kuwahudumia vyema Wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini DCI Ramadhani Kingai alisema kupitia kikao hicho wataweka maazimio ambayo yatakwenda kutekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa lengo la kutoa haki kwa wananchi.
DCI Kingai alisema kikao hicho kitafuatiwa na Kikao cha Watendaji wa Ofisi hizo kutoka Tanzania bara na Zanzibar ambao nao watayapitia kwa kina maazimio yatakayowekwa na kikao hicho cha Menejimenti.



























