Na Mwandishi Wetu
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewekeza zaidi ya Sh.trilioni 6.7 katika sekta ya afya ili kuhakikisha
anamaliza rufaa za wagonjwa wanaotakiwa kwenda kupata tiba nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mbio za Saifee (Saifee
Marathon) zilizoandaliwa na Hospitali ya Saifee na kufanyika katika viwanja vya Green Park Masaki jijini
Dar es Salaam kwa ajili ya kuwezesha upasuaji wa saratani ya matiti.
Katika mbio hizo, Dk. Mollel alimwakilisha Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
“Ili kufikia azma ya Rais wetu Dk. Samia, lazima tushirikiane na sekta binafsi kwa lengo la kuhakikisha rufaa za wagonjwa wa nje zinaisha na kuvutia nchi za nje kufuata huduma za afya nchini kwetu,” alisema.
Alisema Rais Dk. Samia ameboresha miundombinu katika sekta ya afya ikiwemo teknolojia katika sehemu ya
kutolea huduma, upatikanaji wa dawa na kusomesha wataalamu wa afya chini ya Programu ya SamiaScholarship.
Naye Naibu Waziri wa Afya Zanzibar, Hassan Khamisi, alisema kwa upande wa Zanzibar wameanza kushirikiana
na sekta binafsi na Hospitali ya Saifee inasimamia kuhakikisha huduma za afya Zanzibar zinapatikana kwa ufasaha.
“Sisi kama serikali tutahakikisha tunasimamia ubora wahuduma kwa wananchi kwa kushirikiana na sekta binafsi
nchini,” alisema.