Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa, Tanzania inakusudia kujiunga na mkataba wa Wakala wa kimataifa wa Nishati Jadidifu duniani (International Renewable Energy Agency- IRENA) kutokana na faida mbalimbali zinazotokana na mkataba huo ikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha upatikanaji wa nishati safi, salama ya uhakika na gharama nafuu pamoja na kupunguza umasikini na kuleta Maendeleo endelevu.
Naibu Waziri ametoa kauli hiyo Oktoba 20, 2023 jijini Dodoma katika Kikao na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilicholenga kujadili mapendekezo ya Tanzania kujiunga na Mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (IRENA).
Amesema faida nyingine ambazo Tanzania itapata baada ya kujiunga na mkataba wa IRENA ni pamoja na kunufaika na mikopo mbalimbali ya kufanya tafiti, kuibua na kuendeleza miradi ya Nishati Jadidifu inayotolewa kwa nchi wanachama na kupata misaada ya kiteknolojia kwa ajili ya uendelezaji wa nishati Jadidifu.
Amesema kuwa, Nishati Jadidifu ni nishati isiyoisha wakati inapotumika kama vile jua, upepo na nishati ya jotoardhi ambazo ni tofauti na nishati nyingine ambazo huisha mara baada ya kutumika.
“Nishati Jadidifu ndio nishati ya kipaumbele kwa sasa hapa duniani kwa sababu nishati hii ni rafiki kwa Mazingira na bei ya mauzo ya umeme unaotokana na nishati jadidifu ipo chini kuliko umeme unaozalishwa kutokana na nishati zisizo rafiki kwa mazingira.” Amesema Kapinga
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa mkataba wa IRENA hauzuii matumizi ya nishati nyingine kama vile gesi na makaa ya mawe, bali unahimiza matumizi ya nishati mbadala na rafiki kwa mazingira.
“Mfano wa nchi wanachama wa IRENA ambazo bado zinaendelea na matumizi ya nishati nyingine ni pamoja na Urusi, China na Ujerumani ambazo bado zinazalisha na kununua makaa ya mawe na Mafuta,” amesema Mhandisi Mramba
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kupitia kwa Mwenyekiti wake, Mhe. Mathayo David Mathayo wameipongeza Serikali kwa kuwa na mpango huo wa kujiunga na mkataba wa kimataifa wa nishati Jadidifu ambao wameeleza kuwa faida zake ni kubwa ikiwemo suala la msingi la kulinda na kuhifadhi Mazingira.