Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Finland nchini Tanzania pamoja na taasisi ya Protection International Africa imeendesha Mkutano wa Kimkakati na Wadau wa vyombo vya Habari kujadili kuhusu Maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (Media Service Act, 2016).
Mkutano huo umefanyika leo Ijumaa Novemba 3,2023 jijini Dar es salaam na kukutanisha wadau wa vyombo vya habari wakiwemo Wanasheria na Waandishi wa habari.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano huo, Mkurugezi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), Elizabeth Riziki amesema mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji Mradi wa Kufahamu Haki za Binadamu Kupitia Uhuru wa Vyombo vya habari na Marekebisho ya Sheria (Realising Human Rights Through Media Freedom And Legal Reforms) unaotekelezwa na MISA TAN, Ubalozi wa Finland nchini Tanzania na taasisi ya Protection International Africa.
“Mkutano huu wa leo unalenga kujadili Maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (Media Service Act 2016), kupitia maeneo ambayo bado yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa waandishi wa habari na uhuru wa kujieleza ambapo mapendekezo yanayotokana na mkutano huu yatajumuishwa na mapendekezo ya maboresho mengine kutoka Sheria mbalimbali zinazohusiana na uhuru wa kujieleza”, amesema Elizabeth.
Katika Mkutano huo, wadau wa habari wamejadili kuhusu Maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (Media Service Act 2016) na kutoa maoni kuhusu marekebisho ya sheria hiyo.