Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kuwa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 hayataweza kutumika kama jamii haitafahamu mahali yanapopatikana na namna ya kuyatumia katika shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo.
Msigwa amliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi wa mila na desturi yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Alisema matokeo hayo ya sensa na takwimu ni muhimu kwa sababu ndiyo dira inayoongoza katika kufanya maamuzi yote ya msingi yanayohusu mustakabali wa nchi hivyo ni muhimu jamii ikafahamu jinsi ya kuyapata na namna ya kuyatumia.
“Katika kuhakikisha jamii inafahamu matokeo haya ya sensa serikali imetayarisha muongozo wa kitaifa wa matumizi ya matokeo ya sensa ambao umeanisha wadau na njia za kuwafikia kuweza kuwasilisha matokeo haya na kwa kufanya hivyo sera, mipango na shughuli za maendeleo zitahakisi idadi halisi ya watu na mahitaji hatimaye kujibu changamoto za maendeleo zinazowakabili wananchi kwa ufanisi na uhakika zaidi,” alisema Msigwa
Aidha alisema mafunzo hayo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa kwa viongozi wa mila na desturi ni muhimu kwa sababu yatawawezesha kuyafahamu matokeo hayo ya sensa ambayo yanasaidia kuelewa na kuona orodha ya maeneo yanayoyaongoza.
“Matokeo haya yatasaidia pia kujua namna bora ya kuwasiliana na jamii katika kufanya maamuzi wakati wa kutoa ushauri, viogozi hawa wa mila na desturi ni miongoni wa makundi yanayoaminika na serikali,” alisema Msingwa.
Hata hivyo, alisema mafunzo haya yanaumuhimu wa kipekee katika kujenga mustakabali mwema wa maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii na kuongeza kuwa serikali inathamini mchango mkubwa wa viongoni wa mila na desturi.
Naye Kamisaa wa Sensa ya watu na makazi Tanzania bara 2022 ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge, Anna Makinda alisema sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 imefanyika kwa mafanikio makubwa kwani asilimia 99.9 ya watu walijiandikisha.
NBS inawashukuru watu wote waliofanikisha zoezi hili wakiwemo viongozi wa mila na desturi, mchango wa hawa viongozi wetu ulikiwa mkubwa sana ambao umetusaidia kufanikisha,” alisema
Kwa upande wake kiongozi wa machifu nchini, Antonia Sangali alisema wataendelea kushirikiana na NBS ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi za matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.
“Tunaishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutukumbuka machifu kwa kutupatia elimu hii ili na sisi kuipeleka kwa wananchi waweze kuitumia katika shughuli zao za kimaendeleo,” alisema





























