Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amesaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa Kuwait kufuatia kifo cha Amir wa Kuwait, Sheikh Nawaf al-Ahmad Al-Sabah, katika Ubalozi wa nchi hiyo Jijini Dar es Salaam.
Kiongozi huyo alifariki tarehe 16 Disemba 2023 akiwa na umri wa miaka 86 ambapo aliongoza taifa hilo kwa miaka mitatu iliyopita.
Balozi Mbarouk ametoa salamu za pole za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Balozi wa Kuwait nchini, Mhe. Mubarak Mohammed Alsehaijan ambapo amemuelezea kiongozi huyo atakumbukwa daima kama mwanadiplomasia na kiongozi imara aliyejitolea maisha yake katika masuala ya amani.
“Kiongozi huyo atakumbukwa kama kiongozi mahiri wa Kuwait aliyeimarisha ushirikiano wa karibu Kati ya Kuwait na Tanzania,” alisema Balozi Mbarouk.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunapenda kutoa salamu zetu za pole kwa wananchi wa Kuwait kwa kuondokewa na kiongozi bora na mpenda amani. Roho yake Ipumzike mahali pema peponi,” aliongeza Mhe. Balozi Mbarouk
Balozi Mbarouk aliongeza kuwa Daima Serikali ya Muungano wa Tanzania itamkumbuka Hayati Sheikh Nawaf al-Ahmad Al-Sabah kama kiongozi imara na aliyependa amani.