Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mha. Exaudi Fatael Maro, akifungua kikao cha maandalizi ya kongamano hilo, leo, tarehe 21 Desemba 2023 jijini Dodoma, amesema lengo la kukutanisha wadau, ni kujadili na kupata suluhu ya changamoto zinazoikabili sekta ndogo ya gesi asilia kwa upande wa CNG.
“ Ni matarajio yetu kuwa, kupitia kikao hiki, tutaweza kuandaa utaratibu wa utoaji elimu kwa wawekezaji na watanzania kwa ujumla kuhusu CNG.” Alisema.
Mha. Maro amewahisi washiriki wa kikao hicho kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Ardhi, Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam, Mamlaka ya Mapato, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira, Shirika la Taifa la Utafiti wa mafuta na gesi, Shirika la Viwango na EWURA kuimarisha ushikiano na kila taasisi husika kutekeleza wajibu wake ili kufanikisha kongamano hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Gesi Asilia EWURA, Mha. Poline Msuya, ameeleza kuwa, kwa kuwa EWURA ndiye msimamizi wa miundombinu ya huduma ya CNG, itaendelea kutimiza wajibu wa kuhakikisha uwekezaji kwenye sekta hiyo, unafanywa kwa mujibu wa utaratibu ulioanishwa kwenye sheria na kanuni.





























