Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameutaka Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) ukamilishe mchakato wa kupata ithibati ya pili kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Amesema hayo alipofanya Mkutano wa Uwili na Mkuu wa Sekretariati ya Mfuko huo Bw. Mikko Ollikainen pamoja na timu yake pembezoni na Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) unaoendelea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu leo Desemba 5, 2023.
Dkt. Jafo amesema NEMC ambayo ndiye msimamizi wa fedha za mfuko huo nchini Tanzania ilipitiwa na mchakato wa ithibati kwa takriban miaka miwili sasa hivyo inapaswa ikamilishiwe mchakato huo.
Vilevile Waziri Jafo ameisisitiza Sekretariati ya mfuko huo kuongeza kasi katika kupitia taarifa za mwaka za miradi inayoendelea kutekelezwa, kuzipitisha na kuruhusu fedha za mwaka unaofuata kutolewa.
Mkutano huo umeleta manufaa ya haraka ambapo Mfuko umeahidi kutendea kazi masuala hayo na baadhi ya hayo yameanza kushugulikiwa muda mchache baada ya mkutano.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali itaendeelea kuhakikisha taasisi zote zinazoomba usajili katika Mfuko huo zinafanikiwa kupata usajili ili kunufaika na faida zake.





























