MABINGWA wa Afrika, Al Ahly wamewasili Dar es Salaam usiku wa Alhamisi na kupokewa na basi la Kampuni ya Happy Nation Express ambao hutoa huduma za safari za mikoa ya Mwanza, Bukoba, Mbeya, Dodoma na Arusha.
Al Ahly wamekuja tena Tanzania kwa ajili ya mchezo wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Yanga SC utakaochezwa Saa 1:00 usiku Jumamosi Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Wanarejea Dar es Salaam baada ya mwezi mmoja na ushei tangu wacheze na timu nyingine ya Tanzania, Simba SC Oktoba 20 hapo hapo Uwanja wa Mkapa na kutoa sare ya kufungana mabao 2-2 katika mchezo wa Robo Fainali ya African Football League (AFL).
Al Ahly iliitoa Simba kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya kutoa tena sare ya 1-1 kwenye mchezo wa marudiano Oktoba 24 Uwanja wa Kimataifa wa Cairo Jijini Cairo nchini Misri.
Mechi ya kwanza wa Kundi D Al Ahly ilishinda 3-1 dhidi ya Medeama ya Ghana Jijini Cairo Jumamosi, wakati Yanga ilifungwa 3-0 na CR wenyeji, Belouizdad Jijini Algiers nchini Algeria Ijumaa iliyopita.