UKITAJA wasanii wa kike wanaofanya vizuri katika anga ya miondoko ya Bongo Fleva, hutaacha kutaja jina la Lulu Euggen ‘Amber Lulu’ kutokana na umahiri wake katika kuimba.
Umahiri huo unasababisha kuendelea kudumu katika muziki huo wa kizazi kipya na kupata idadi kubwa ya mashabiki hadi sasa.
Japokuwa kuna ushindani mkubwa katika bongo fleva, Amber Lulu anaendelea kufanya vizuri kutokana na kuachia nyimbo kali ambazo zinatingisha katika stesheni mbalimbali nchini.
Msanii huyo ametoa nyimbo mbalimbali zikiwemo ‘Walete’, ‘Nimeachika’, ‘Watakoma’, ‘Kanipa Yote’, ‘Sigino’, ‘Kiboko Yao’, ‘Machozi’, ‘Kumoyo’, ‘Only You’, ‘No Control’ na ‘Vuruga’ ambazo zinafanya vizuri katika medani ya muziki wa bongo fleva.
Amber Lulu anasema kwa sasa staili yake mpya ya muziki wa amapiano imemuongezea idadi ya mashabiki ambao wamezidi kumwamini kadiri siku zinavyosonga mbele.
Msanii huyo anasema kubadilisha staili za muziki inamsaidia kupiga hatua na kupata mashabiki wapya.
“Nashukuru Mungu muziki wa amapiano umeniongezea mashabiki wapya kutokana na kazi ninayofanya…napokea maoni mengi,” anasema na kuongeza.
“Pia muziki huu umenipa jina kubwa sasa naitwa ‘Queen of Amapiano’ kwa sababu nafanya vizuri na kuwa na morali ya hali juu kipindi nafanya muziki wa amapiano,” anasema Amber Lulu.
Anasema kuwa kupitia staili hiyo mpya ya muziki wake, anaamini atatoa ngoma mbalimbali ili kuwafurahisha mashabiki wa burudani.
Ameahidi kuachia nyimbo nyingine kupitia staili ya amapiano inayotamba katika baadhi ya nchi za Afrika.
“Mashabiki wategemee mambo mazuri kutoka kwangu kwa aina hii ya amapiano wategemee kusikia muziki wa aina yoyote kama singeli au taarabu kutokana na morali yangu, ndiyo maana wananiita Queen of Amapiano,” anasema Amber Lulu.
Msanii huyo anasema maisha yake yamebadilika kwa asilimia kubwa kutokana na kuachana na mambo ya starehe na kuzingatia kuendelea kuchapa kazi.
Anasema mtoto wake ‘Arianna’ amebadilisha maisha yake jambo ambalo anafarijika kuona anasimama kama mama katika maisha ya mwanawe.
“Maisha yangu sasa yamebadilika baada ya kupata mtoto, hapo awali nilikuwa nafanya starehe ila kipindi hiki naangalia kazi na kuwa karibu na mwanangu,” anasema Amber Lulu.
Ameeleza mara nyingi anapokuwa nyumbani anatumia muda huo kuwa karibu na mtoto wake ili kutaka kufahamu tabia na kipaji alichojaliwa nacho.
Amesema kwa kuwa kipaji cha mtoto kinaanzia akiwa mtoto, hivyo ni wajibu wa wazazi kukaa karibu na watoto wao ili kutambua wamejaliwa nini.
“Nchi za mwenzetu wanaendeleza kipaji cha watoto wao wakiwa bado wadogo, ndiyo maana tunaona vipaji mbalimbali na wanafanikiwa kwa sababu wanaanza mapema,” anasema Amber Lulu.
Msanii huyo amewaomba mashabiki wake kuendelea kuwa naye bega kwa bega katika kazi zake ili kumwezesha kufika mbali na kukuza soko la muziki nchini.
“Nawashukuru mashabiki wangu kwa kuendelea kuniamini, pia nawaomba waendelee kunisapoti ili kufika mbali na kutangaza taifa kupitia kipaji changu,” anaongeza Amber Lulu.
Na AMINA KASHEBA