MKAZI wa Kibamba- Kibwegere, Dar es Salaam, Julias Nyaki au Tall Myama, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kujibu shtaka la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.
Nyaki (33) alifikishwa Mahakamani hapo na kusomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenda, mbele ya Hakimu Mkazi, Lilian Silayo.
Mwaitenda alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Juni na Julai, mwaka huu, eneo la Kibamba- Kibwegere, Wilayani Ubungo, ambapo alimbaka mtoto huyo (jina tunalihifadhi).
Mshitakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu alimweleza mshtakiwa shtaka linalomkabili linadhaminika na kumtaka kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika ambao watatia saini dhamana ya sh. milioni mbili.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana, baada ya kutimiza masharti hayo na shauri liliahirishwa hadi Septemba 27, mwaka huu, litakapopelekwa kwa usikilizwaji wa awali.
Wakati huo huo, mkazi wa Kijitonyama, Kinondoni, Dar es Salaam, Athuman Ally (31), alifikishwa Mahakamani hapo, kujibu shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wakili wa Serikali, Veronica Mtafya, alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Sifa Jacob, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, Juni 26, mwaka huu, eneo la Kijitonyama, Kinondoni.
Inadaiwa mshtakiwa aliiba simu aina ya tekno F1 yenye thamani ya sh. 120,000, mali ya Somoe Salumu na kwamba kabla na baada ya kutenda kosa hilo, alimtishia Somoe kwa kisu ili kujipatia mali hiyo.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu huyo alimweleza mshtakiwa kuwa shauri linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo alirudishwa rumande hadi Oktoba 4, mwaka huu.
DEBORA BONIFACE, MEKI KIPALILO (TUDARC0) na HAWA NGADALA



























