Askofu Mkuu wa Kanisa la Naioth Gospel Assembly, Dk. David Mwasota, amelipongeza Taifa kwa kufikisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuzaa Tanzania. Akitoa pongezi hizo, Askofu Mwasota amesema, ni rahisi kuungana lakini si kitu rahisi hata kidogo kuuishi muungano kwa amani na furaha kama ilivyo kwa Jamhuri yetu.
Askofu Mwasota aliyasema hayo alipoongea na gazeti la Uelekeo ofisini kwake yalipo Makao Makuu ya kanisa hilo, maeneo ya Makuburi, External jijini Dar es Salam.
Askofu amefafanua kuwa, suala la Muungano ni dhana ya ki- Biblia na muasisi wake ni Mungu. Yeye mwenyewe (Mungu) pamoja na wanadamu kuasi na kukengeuka mara kwa mara aliendelea kuwajia na kuungana nao.
Pamoja na hayo ameanzisha Miungano ya aina mbalimbali inayohusisha watu kuja pamoja kama vile ndoa, jumuiya nk. Hii inaonesha kuwa, kuja pamoja ni suala la ki Mungu kabisa.
Licha ya hayo yote, bado suala la kuendelea kukaa pamoja limekuwa kitu kigumu ndiyo maana sehemu mbalimbali ambazo watu wameungana kumekuwa na migogoro isiyoisha na hata watu hao kuvurugana, kutoelewana na kusambaratika.
Askofu Mkuu, Dk. David Mwasota anaupongeza sana Muungano huu kwani umeendelea kuwa imara, wenye manufaa, wenye amani na utengamano siku zote.
Askofu Mwasota ameeleza kuwa miaka mingi tumesikia habari za kero za Muungano ambazo sasa haziitwi kero tena bali zinaitwa hoja za Muungano lakini pamoja na hoja hizo hatujawahi kuhitilafiana wala kugombana. Hoja za muungano zimeendelea kutambuliwa, kupokelewa na serikali zote mbili, kutafutiwa ufumbuzi kitaalamu na kijamii na hatimaye zimeendelea kupungua siku baada ya siku.
Sambamba na hayo, Askofu Mwasota amefafanua kuwa, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa Bungeni na Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk. Suleiman Jafo, tarehe 9 Februari mwaka huu ni kwamba, kati ya hoja 25 za Muungano mwaka 2006, hoja 22 zimetatuliwa na kuondolewa kwenye hoja za Muungano na kubakia 3 tu.
Huu ni umahiri mkubwa na tunaamini kuwa Mungu anahusika sana kutoa hekima kwa viongozi wetu kuendelea kudumisha Muungano wetu. Hivyo amewataka watanzania, wanasiasa, wanaharakati na wachambuzi wa kisiasa kuutazama Muungano huu kwa jicho la hekima hiyohiyo maana ukiingiza uchambuzi wa kibinadamu na kutaka kuiga wengine, tutaingiza chokochoko na migogoro isiyo na maana. Kama Muungano wetu umeendelea vizuri, amani ipo, basi tuudumishe.
Akihitimisha hayo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Naioth Gospel Assembly, Dk. David Mwasota alisema anauona Muungano ukichanua zaidi, ukipata maendeleo makubwa na kustawi sana miaka michache ijayo kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali zote mbili kwa sasa.
Marais wetu wote wawili (Dk. Samia na Dk. Mwinyi) ni watu wa amani, majasiri na wachapakazi. Askofu Mwasota anaeleza kuwa, wananchi wa Tanzania pia ni waelewa sana na zaidi sana falsafa ya 4R (Four R) za Rais Samia, zitauweka salama zaidi Muungano wetu kama wote tutapokea na kuishi hekima hii ambayo Mungu anatupa.
Kupitia Falsafa hii, sasa hivi tunaridhiana kupitia “Reconciliation”, Tunastahimiliana kupitia “Resilience”, Tunabadilika kuwa bora zaidi kupitia “Reform” na Tunajenga upya kupitia “Rebuilding”.