Hayo yalielezwa na Katibu wa Sungusungu, Mtaa wa Sangilwa, Mihayo Senya, wakati akisoma taarifa ya mapato na matumizi ya jeshi hilo kwa wananchi katika kipindi cha miezi sita tangu waingie madarakani ikiwa ni utekelezaji wa kanuni walizojiwekea.
Amesema katika kipindi cha miezi sita, watu zaidi ya 20 walikamatwa kwa makosa mbalimbali na kutozwa faini kama utaratibu wa jeshi hilo unavyotaka kwa mtu anayethibitika kufanya makosa.
“Sultan Seif aliingilia majukumu ya sungusungu alitozwa faini sh. 100,000, Lucia Leonard aliiba kuku wa jirani yake alitozwa sh. 100,000, Pili Kashindye alikodisha miti ya embe mara mbili aliamriwa kulipa sh. 100,000, Manyenye Tego aliiba godoro la jirani yake alitozwa faini 100,000,” alisema.
Senya alisema faini hizo zinatozwa kwa mujibu wa sheria za mtaa walizojiwekea, huku baadhi ya makosa wahusika wamelipishwa faini za mifugo ikiwemo ng’ombe na mbuzi na fedha hizo zimekuwa zikitumika katika miradi ya maendeleo.
Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sangilwa, Sultan Seif, aliwataka viongozi wa sungusungu kuacha kunyanyasa wananchi kwa kuwatoza faini kandamizi, badala yake wanaobainika kufanya makosa makubwa ni bora wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
“Acheni kusikiliza kesi ambazo ziko juu ya uwezo wenu mnatoza faini kandamizi ambazo zinaleta malalamiko, mtu anaiba kuku wa sh. 20,000 anatozwa sh. 100,000 hili halikubaliki sheria hizi lazima tuzibadilishe,” alisema.
Kwa upande wake, Japhet Masonga mkazi wa mtaa huo, alidai sungusungu katika eneo hilo wamekuwa wakiwaonea wananchi kwa kuwatoza faini kubwa hivyo kuiomba serikali kuingilia kati suala hilo.
“Nilikamatwa kwa kutoshiriki katika ulinzi usiku nikatozwa faini sh. 100,000, ukiwauliza mapato na matumizi unakuwa adui yao, wananchi katika mtaa huu wanaishi kwa kuwaogopa baadhi ya viongozi wa mtaa huu ambao wamekuwa miungu watu,” alilalamika.
Mwenyekiti wa Wazee wa Kata ya Mondo, Makoye Gilli, alisema vitendo vya wizi wa mazao vimeanza kushamiri katika mtaa huo baada ya kikundi kisichofahamika kuwateka vijana waliokuwa wakisafirisha mpunga.
“Sangilwa kwa kipindi cha miezi mitatu matukio manne ya utekaji yameripotiwa ikiwemo wizi wa mbuzi, vitunguu na mpunga huku wahusika wakishindwa kujulikana na kuwasababishia wamiliki wa mali majeraha, vitendo hivi havikubaliki serikali iingilie kati suala hili haraka,” alisema.
SALVATORY NTANDU, Kahama