WAZIRI wa Maji Juma Aweso, ameongoza kazi ya utiaji saini mikataba ya dira za maji za malipo kabla ya matumizi na kutangaza bei ukomo za huduma hiyo maeneo ya vijijini.
Pia, aligawa pikipiki 250 kwa ajili ya watendaji wa wizara hiyo.
Aweso aliongoza kazi hiyo jijini Dodoma wakati wa hafla ya upokeaji wa taarifa ya utendaji ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Kuhusu utendaji kazi wa RUWASA, amesema serikali inashuhudia kazi kubwa iliyofanywa na wakala huo katika kutekeleza miradi ya maji na kuwezesha mingine maeneo ya vijijini ili kutekelezwa kwa ubora tofauti na miaka iliyopita kabla ya uanzishwaji na wakala huo.
“Kwa awamu hii, tumetekeleza bajeti ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande wa wizara ya maji kwa asilimia 95, tofauti na miaka ya nyuma tulipokuwa tukitekeleza asilimia 50 hadi 51, ni jambo la kijipongeza sana,” alisema Aweso.
Alisema tukio la uwepo wa dira za maji za malipo kabla ya matumizi ni mapinduzi makubwa kwa kuwa, jambo hilo limepigiwa kelele kwa muda mrefu na watumiaji wakiwemo wabunge kupitia Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.
“Tunashukuru uamuzi mliofikia wa kwenda kutumia vyuo vya elimu ya ufundi katika kufanikisha utengenezaji wa dira za maji, haya ni mageuzi makubwa, tunaona ambavyo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwamba, imekuwa msaada katika kuibua wataalamu na kufanya bunifu mbalimbali,” alisema.
Aweso alisema hatua ya kutangaza bei kikomo ya maji vijijini ni suala la kihistoria kwa sababu ni jambo lililokuwa na changamoto kubwa kwa muda mrefu.
Akizungumzia vitendea ambavyo ni pikipiki 250 kwa vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO), aliwataka kuhakikisha wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, si kutumia kama bodaboda.
Na HAPPINESS MTWEVE, Dodoma