Na NASRA KITANA
UONGOZI wa Klabu ya Azam FC, umetamba kuwa upo kwenye mpango wa kuwapiku vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga, ili waweze kukaa juu yao.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Azam ipo nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi sita ambapo imeshacheza mechi 24 wakati Yanga ikiwa kileleni kufuatia kucheza mechi 23 na pointi 50, Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 44.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ amesema tangu ligi ianze lengo lao ni kuhakikisha wanamaliza nafasi mbili za juu na hilo linawezekana kwani lipo ndani ya uwezo wao.
Amesema wao hawana presha na aliyekuwa nyuma yao ila wanaiangalia Yanga ambao ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwani siku chache zilizopita hawakuwa na matokeo mazuri.
“Msimu huu tunajambo letu, ambapo iwe isiwe lazima tumalize nafasi mbili za juu katika msimamo wa Ligi Kuu na suala hilo lipo ndani ya uwezo wetu kwani tunaamini litatimia,” Zaka.
Ameongeza kuwa, kwa sasa Ligi Kuu imesima kwa muda kupisha mandalizi ya michezo ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ila timu yao bado inaendelea kupigwa msasa na benchi la ufundi la kikosi hicho linaangalia jinsi ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mechi zilizopita.