POLISI Mkoa wa Manyara, inamshikilia mzee wa miaka 57 kwa tuhuma za kuwabaka mabinti zake watatu, wenye umri wa miaka 15, 17 na 18.
Tukio hilo linadaiwa kutokea wiki iliyopita katika Kijiji cha Ndaleta, Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara.
Kutokana na tukio hilo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, imetoa tamko kuhusu kitendo hicho na kuonyesha kusikitishwa kwake na kuwaomba wananchi kuungana na kupinga ukatili wa makundi yote.
Tamko hilo lilitolewa Januari 17, 2022 kupitia taarifa kwa umma iliyotiwa saini na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Prudence Constantine na kubainisha kuwa, watoto walishapatiwa huduma za kiafya, msaada wa kisaikolojia na kijamii.
“Hivi karibuni katika jamii kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili kwa makundi yote wakiwemo watoto, ambapo wiki iliyopita limeripotiwa tukio la baba mwenye umri wa miaka 57 kudaiwa kuwabaka mabinti zake watatu huko mkoani Manyara katika Wilaya ya Kiteto, Kijiji cha Ndaleta. Watoto hao wakiwa na umri wa miaka 15,17 na 18,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
“Wizara imesikitishwa na taarifa za tukio hilo na inapenda kutoa taarifa kuwa, tayari mtuhumiwa ameshakamatwa na vyombo vya usalama yupo mikononi mwa polisi kwa utaratibu zaidi wa kisheria,”alisema.
Ilisema wizara hiyo iliwasisitiza wananchi kuungana kupinga ukatili wa makundi yote na kutoa taarifa mapema katika vyombo vya serikali na vya kijamii vinavyotoa msaada wa haraka pale tukio linapotokea au viashiria vyovyote vya namna hiyo.
Taarifa hiyo iliwaomba viongozi wa dini wakati wa ibada watumie jukwaa hilo, kuendelea kukemea vitendo vya ukatili ili kuleta amani na utulivu katika jamii.
Hata hivyo, ilisema wizara kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuimarisha mifumo ya kudhibiti ukatili katika jamii.
NA MWANDISHI WETU



























