NIBAJETI ya wananchi. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, kuwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/2023 ya sh. trilioni 41.01
Bajeti hiyo, imetoa nafuu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wananchi wa kawaida katika mafuta ya kupikia, petroli, mbolea, sukari na kuondoa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Akiwasilisha bajeti hiyo jana baada ya Bunge kujadili kwa kirefu bajeti za kisekta, Dk. Mwigulu alisema katika bajeti hii, Serikali imependekeza kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi, ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya Sheria mbalimbali na kurekebisha taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato ya Serikali.
Dk. Mwigulu alisema marekebisho hayo, yamezingatia dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa na mfumo wa kodi ambao ni tulivu na wa kutabirika, ambapo yanatarajiwa kujibu maswali na kukidhi kiu ya Watanzania.
Alisema yanalenga kuchachua shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ndani ya nchi kwa kuweka mkazo katika sekta za kimkakati kama vile kilimo, ufugaji na uvuvi, miundombinu ya umeme, uchukuzi na usafi rishaji na sekta za kijamii za elimu na afya ili kuboresha uzalishaji, kukuza uchumi jumla, kukuza ajira na hatimaye kupunguza ukali wa maisha ya wananchi.
Waziri huyo alisema Serikali inafanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ili kuiwezesha Serikali kukusanya Kodi ya Ongezeko la Thamani katika biashara mtandao (digital services) bila kuathiri uwajibikaji chini ya Sheria ya Kodi ya MAPATO, SURA 332.
Waziri Mwigulu aliongeza kwa kusema, marekebisho hayo yanalenga kurahisisha utaratibu wa usajili wa walipakodi wanaotoa huduma za kidijitali bila kuwa na makazi nchini (simplifi ed registration).
“Hatua hii, inalenga kwenda pamoja na mwamko wa shughuli za kibiashara duniani zinazofanyika kwa njia ya mtandao. Hatua hii, inatarajiwa kuiongezea Serikali mapato ya sh. milioni 34,240” alisema.
Vilevile, alisema Serikali inapendekeza kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani katika simu janja za mkononi (Smartphones) HS code 8517.12.00, vishikwambi (Tablets) HS Code 8471.30.00 au 8517.12.00 na Modemu HS Code 8517.62.00 au 8517.69.00.
Alisema uamuzi huo, unakuja kwa sababu msamaha husika haujawezesha kupatikana kwa bidhaa hizo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake, unawanufaisha wafanyabiashara.
Kufuta msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye huduma za kukodi ndege (air charter services) kwani huduma hizi hutolewa kibiashara kama huduma za kukodi vyombo vingine vya usafi ri ambazo kisheria hulipiwa Kodi ya Ongezeko la Thamani.
Alisema hatua zote za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 87,523.
Dk. Mwigulu alisema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kwa Kufanya marekebisho kwenye Jedwali la Kwanza la Sheria ya Kodi ya Mapato. “…
Tunafanya hivi ili kuweka kiwango cha asilimia 3.5 kwa walipakodi wenye mauzo yanayozidi sh. milioni 11,000,000, lakini yasiyozidi sh. milioni 100,000,000 kwa mwaka, kwa lengo la kuweka uwazi na kurahisisha makadirio na ulipaji wa kodi.
“Hatua hii itaongeza ulipaji kodi wa hiari na hivyo kuongeza mapato ya Serikali ambayo yanatarajiwa kuongezeka kwa sh. milioni 60,413.37.
“Pamoja na pendekezo hili, inapendekezwa kufanya maboresho kwenye mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kuwezesha malipo kufanyika kwa njia ya simu,” alisema.
URAHISI WA KUPATA MIKOPO
Dk. Mwigulu alisema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kubainisha kuwa mikopo mbadala iliyoidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayotolewa na benki kwa wateja wake ambayo inahusisha ununuzi na uuzaji wa mali anazozihitaji mteja kwa faida inayowekwa juu ya gharama ya mali ni sawa na mikopo mingine ya kawaida.
“Hatua hii haimwondolei muuzaji wajibu wa kulipa kodi ya ongezeko la mtaji kwa mujibu wa Sheria katika muamala wa mauzo ya mali kwa mteja wa benki aliyenunua mali hiyo kupitia utaratibu wa mkopo mbadala.
“Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa, Watanzania wote wanaweza kupata mikopo katika taasisi za fedha ikijumuisha wale ambao hawakubaliani na utaratibu wa riba,” alisema.
Aliongeza kuwa, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Kifungu cha 10 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ili kumpa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, mamlaka ya kusamehe kodi ya mapato kwa wawekezaji mahiri maalumu baada ya kuidhinishwa na NISC kwa mujibu wa kifungu cha 20(8) cha Sheria ya Uwekezaji Sura ya 38, pamoja na kupata ridhaa ya Baraza la Mawaziri.
“Lengo la hatua hii ni kufanikisha maendeleo ya sekta ya uwekezaji nchini na kuondoa mgongano wa kisheria kuhusu utoaji wa vivutio vya ziada vya kikodi kati ya Sheria ya Uwekezaji na Sheria ya Kodi ya Mapato,” alisema.
Alisema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuondoa msamaha wa kukata Kodi ya Zuio kwenye malipo ya upangishaji nyumba, vyumba na majengo ya biashara.
Aidha, alisema Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato ataingia makubaliano ya uwakala na Ofi si ya Rais – TAMISEMI juu ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi hii.
Kusamehe Kodi ya Ongezeko la Mtaji kwenye uhamishaji wa haki na taarifa za madini kwenda kwenye Kampuni za Ubia zinazoundwa baina ya Serikali na wawekezaji na uhamishaji wa hisa (Free Carried Interest) kutoka Kampuni ya Ubia kwenda kwa Serikali.
“Hatua hii inalenga kusaidia Serikali kutekeleza majukumu yake ya kimkataba na kuhakikisha kuwa uhamishaji na ubadilishaji wa haki na taarifa za madini unafanyika kwa wakati,” alisema.
Aliongeza: “Serikali inapendekeza kusamehe kodi ya Ongezeko la Mtaji kwenye hisa ambazo Serikali imepata kupitia Msajili wa Hazina. Lengo la hatua hii ni kutatua changamoto zilizopo na kuhakikisha kuwa zoezi la ubadilishaji umiliki wa hisa hizo linafanyika kwa wakati.
“Kusamehe kodi ya zuio kwenye Kuponi za Hati Fungani za Makampuni na Manispaa (Coupon for corporate and municipal bond).
“Pendekezo hili linalenga kuongeza vyanzo mbadala vya kugharamia miradi ya maendeleo (alternative fi nancing),” alisema.
Kupunguza kiwango cha kodiya zuio kwenye tasnia ya fi lamu kwa malipo yanayofanyika kwenda kwa watoa huduma wa nje ya nchi kutoka asilimia 15 hadi asilimia 10.
“Lengo la hatua hii ni kukuza tasnia ya fi lamu na kuchochea uhamishaji wa ujuzi kwenye tasnia hiyo kwa lengo la kuongeza ajira na kuboresha maisha.
“Kutoza Kodi ya Mapato ya asilimia 2 kwenye malipo yanayofanywa kwa watoa huduma za kidijitali wa kigeni. Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za kodi.
“Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 4,889.35” alieleza.
Pia, alisema Serikali inapendekeza kutoza Kodi ya Zuio kwa kiwango cha asilimia mbili katika malipo ya wachimbaji wadogo wa madini (Small Scale Miners).
Dk. Mwigulu alisema hatua hii inalenga kuweka utaratibu maalumu wa utozaji kodi kwa wachimbaji hao na kutatua changamoto zilizopo kwenye ukusanyaji kodi katika sekta hiyo.
“Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 37,290.40,” alisema.
“Kutoza kiwango cha mfuto (fl at rate) cha sh. 3,500,000 ikiwa ni kodi ya mapato inayopaswa kulipwa kwa kila magari ya mizigo na mabasi ya abiria kwa mwaka.
Alisema Serikali inapendekeza kuanzisha utaratibu wa kutoza kodi ya awali ya mapato (advance income tax) ya sh. 20 kwa lita kwa wafanyabiashara rejareja wa mafuta ya petroli nchini itakayokusanywa na waingizaji wa mafuta hayo kwa jumla na kulipwa Serikalini.
USHURU WA BIDHAA
Waziri Dk. Mwigulu alisema, kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa kifungu cha 124(2), marekebisho ya viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa (specifi c duty rates) kwa bidhaa zote zisizo za petroli yanaweza kufanyika kila mwaka ili kuviwianisha na mfumuko wa bei na viashiria vingine vya uchumi jumla.
Hata hivyo, alisema kutokana na biashara za bidhaa hizo kuzorota kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na kupanda bei kwa bidhaa za mafuta, Serikali inapendekeza kutokufanya mabadiliko ya viwango maalumu vya Ushuru wa Bidhaa kwa bidhaa zote zisizo za petroli.
Aidha, alisema hatua hiyo inazingatia kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei nchini na azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, hivyo kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, kuvilinda na hatimaye kukuza ajira na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa.
Waziri Mwigulu alisema: “Ninapendekeza pia kufanya marekebisho ya Ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa zifuatazo; Kupunguza ada ya leseni kwa wazalishaji na waingizaji wa bidhaa zinazotozwa Ushuru wa Bidhaa kutoka sh. 500,000 hadi sh. 300,000.
“Hatua hii inalenga kuwapa unafuu wazalishaji na waingizaji wa bidhaa hizo pamoja na kusaidia kurejesha ukuaji wa Sekta baada ya athari za uviko-19 na athari zinazotokana na msukosuko wa kiuchumi duniani.
“Hatua hii inatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa sh. milioni 77.4. Utaratibu wa ukusanyaji wa kodi kwenye vitenge unafanywa na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania chini ya Sheria ya Pamoja ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004;
“Kusamehe Ushuru wa Bidhaa kwenye vifungashio vya maua, matunda, na mbogamboga vinavyotambulika kwa HS Codes 3923.29.00 (puneet, plastic cryovac bags, modifi ed atmosphere packaging – MAP bags, plastic sleeves, perforated bags, poly packaging bags), HS Code 3921.12.90 (cling fi rm), HS Code 3902.90.00 (plastic liners).
“Lengo la hatua hii ni kuwapunguzia gharama wazalishaji wa matunda, mbogamboga na maua, na kuongeza usafi rishaji wa bidhaa hizo nje ya nchi na hivyo kuongeza fedha za kigeni. Hatua hii inatarajia kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 653.12” alisema.
Dk. Mwigulu alisema Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa bidhaa wa sh. 700 kwa kilo ya bidhaa za sukari (sugar confectionery) zinazoingizwa kutoka nje ya nchi na sh. 500 kwa kilo ya bidhaa za sukari zinazozalishwa hapa nchini zinazotambuliwa kwa HS Code 1806.31.00, 1806.32.00, 1806.90.00, (chokoleti), 1905.31 (biskuti) na 1704 (chingamu).
Alisema viwango tofauti vinapendekezwa ili kulinda viwanda vya ndani na kwamba hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa sh. milioni 34,453.87; na kutoza Ushuru wa Bidhaa kwenye betri za maji (Leadacid battery) kwa kiwango cha asilimia 5 zinazotambuliwa kwa HS Code 8507.10.00, na 8507.20.00.
“Hatua hii inalenga kupunguza madhara ya mazingira yanayosababishwa na matumizi ya bidhaa hizo. Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa sh. milioni 1,864.85;
“Hatua hizi za Ushuru wa Bidhaa kwenye bidhaa zisizo za petroli kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 50,292” alieleza Waziri Mwigulu.
Kadhalika aliongeza: “Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438 Mheshimiwa Spika, Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Usimamizi wa Kodi, SURA 438 ili kumrejeshea Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha na Mipango mamlaka ya kusamehe riba na adhabu baada ya kushauriwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Vilevile alisema, kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, SURA 290 Serikali inapendekeza kugawanya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri katika mchanganuo wa asilimia 5 kwenye miundombinu na masoko ya machinga, asilimia 2 kwa ajili ya mikopo kwa vijana, asilimia 2 kwa ajili ya wanawake na asilimia 1 kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
FIDIA KWA WAFANYAKAZI
Dk. Mwigulu alisema kupitia Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263, Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwa kupunguza kiwango cha mchango kwa sekta binafsi kutoka asilimia 0.6 inayotozwa sasa hadi asilimia 0.5 ya mapato ghafi ya wafanyakazi.
MADINI
Waziri Mwigulu alisema Sheria ya Madini, SURA 123 Serikali inapendekeza kuifanyia marekebisho kwa kupunguza kiwango cha mrabaha kutoka kwenye makaa ya mawe yanayotumika kama malighafi ya kuzalisha nishati viwandani kutoka asilimia 3 hadi asilimia 1.
“Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji viwandani, kuchochea uwekezaji zaidi na kukuza ajira,” alisema na kuongeza: “Tunapendekeza kupunguza kiwango cha kutoza mrabaha (royalty) kutoka asilimia 6 hadi asilimia 4 kwa dhahabu inayouzwa kwenye vituo vya kusafi shia madini (refi nery centres).
KOROSHO
Alisema katika Sheria ya Korosho, Namba 18 marekebisho yanayopendekezwa yanagusa mapato yatokanayo na tozo ya kusafi risha korosho ghafi nje ya nchi ili yagawanywe kwa utaratibu wa asilimia 50 ipelekwe Wizara ya Kilimo kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo na Mfuko wa Kilimo (ADF); na asilimia 50 ipelekwe mfuko mkuu wa Serikali.
Lengo la hatua hii ni kuchochea maendeleo ya Sekta ya kilimo na kusaidia upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya ruzuku na tafiti.
TOZO ZA MIAMALA
Waziri Mwigulu alisema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa kwa kupunguza tozo ya muamala kutoka kiwango kisichozidi sh. 7,000 hadi kiwango kisichozidi sh. 4,000 katika kila muamala wa kutuma au kutoa pesa.
“Punguzo hili ni sawa na asilimia 43 ya kiwango cha sasa. Sambamba na hilo, napendekeza kuongeza wigo wa tozo hiyo ili kuhusisha miamala yote ya kielektroniki.
Lengo la hatua hii ni kupunguza makali ya maisha kwa Mtanzania.
MIKOPO
Waziri Mwigulu alisema: “Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania kwa kuweka kiwango cha ukomo wa Serikali kukopa kuwa kiasi kisichozidi asilimia 18 ya mapato ya ndani yaliyoidhinishwa katika mwaka husika badala ya kiwango cha sasa cha moja ya nane ya mapato ya ndani yaliyokusanywa katika mwaka uliotangulia.
MATUMIZI YA MAGARI KUDHIBITIWA
Aidha, serikali imesema katika mwaka wa fedha 2022/23, itabana na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima katika magari ya serikali ambapo sh. bilioni 500, zitaokolewa kwa mwaka.
Katika kutimiza azma hiyo, alisema serikali inatarajia kudhibiti ununuzi na matumizi ya magari kwa kuzingatia Waraka wa Rais Namba moja wa mwaka 1998, kuhusu hatua za kubana matumizi ya serikali na Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Namba mbili wa mwaka 2021, kuhusu utaratibu wa kutumia magari, aina na stahili za magari kwa viongozi katika utumishi wa umma ili kubana matumizi.
Dk. Mwigulu alisema baadhi ya maeneo yenye gharama kubwa kwa serikali ni ununuzi wa magari, mafuta ya uendeshaji, vipuri na matengenezo.
Alibainisha hatua za muda mfupi zitakazochukuliwa ni kupunguza safari za ndani na nje, kukata fedha za ununuzi usio wa lazima, kupunguza ukubwa wa uwakilishi katika mikutano ya ndani na nje na tutapimiana mafuta ya magari ya serikali kila mwezi kufuatana na shughuli za lazima.”
Alifafanua kuwa, utaratibu huo, unatumika kwa wabunge na hawajaacha kufanya shughuli majimboni mwao, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wanapimiwa, baadhi ya Taasisi za Umoja wa Mataifa (UN) wanapimiwa.
Ili kutekeleza hilo, alimwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali, afanye uchambuzi wa wastani wa mahitaji ya mafuta kufuatana na aina ya majukumu, ulazima wa majukumu na ngazi katika utumishi.
Kwa upande wa hatua za muda wa kati na muda mrefu, waziri huyo alipendekeza serikali kubadili utaratibu uliopo kwa kuwakopesha magari watumishi wenye hadhi ya kuwa na gari la serikali, wafanye matengenezo wenyewe, wanunue vipuri na masuala ya mafuta yaangaliwe kwa utaratibu utakaoonekana unafaa.
Alisema kwa sasa, serikali ina magari zaidi ya 15,742, pikipiki 14,047 na mitambo 373 na inatumia zaidi ya sh. 558,453,134,226.05 kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa magari, mafuta ya uendeshaji, vipuri na matengenezo.
Alieleza kuwa, ukiondoa vyombo vya ulinzi na usalama na Mahakama, upande wa serikali watabaki viongozi wakuu wa wizara, mashirika, wakala, mikoa, wilaya na miradi ambao wasimamizi watakuwa eneo la mradi.
“Watumishi wengine wenye stahili ya gari la serikali watakopeshwa, watumie magari yao, watasimamia vizuri matumizi, matengenezo, mafuta na vipuri.
Tutaondoa utaratibu uliozoeleka, dereva na gari anapitishwa chini, bosi anapanda ndege mpaka Mwanza au Mbeya kutoka Dar es Salaam na kurudi.
“Kuna utafi ti wa siri ulifanywa, kwa siku moja yalibainika magari ya serikali yaliyotoka Dodoma kwenda Dar es Salaam yalikuwa 132 na yaliyokuwa yanatoka Dar es Salaam yakipishana kuja Dodoma, yalikuwa 76, na mengine manane yalikuwa yamepinduka. Je, kwa mwezi ni gharama kiasi gani?,” alihoji.
Alifafanua kuwa, kwa utaratibu huo, gharama za matumizi ya magari serikalini zitakuwa sh. bilioni 50.508.
“Zaidi ya sh. bilioni 500, zitaokolewa na kuelekezwa kwenye ununuzi wa dawa muhimu hospitalini, kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya kati na kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema. Aliongeza:
“Tumezidi kupenda ubosi, magari 17 makubwa kwa kila mtu serikalini, matumizi ya starehe, wakati katika nchi yetu, bado kuna watu wanapata shida kupata mlo mmoja. Rais Samia, ameielekeza Wizara ya Fedha na Mipango, ifanyie kazi jambo hili la kuelekeza fedha katika matumizi ya msingi tu.”
WAKUU WA MASHIRIKA YA UMMA KUFANYIWA USAILI
Serikali imependekeza nafasi za wakuu wa mashirika ya umma kuanza kutangazwa pindi zinapokuwa wazi na waombaji wafanyiwe usaili kwa ushindani, badala ya kuteuliwa.
Imesema waombaji wenye sifa, watafanyiwa upekuzi kisha kufanyiwa uteuzi na kupewa mkataba wenye malengo yanayopimika.
Waziri Dk. Mwigulu, alisema mashirika mengi yamekuwa mzigo kwa serikali ambapo yanategemea ruzuku kutoka serikalini ili yajiendeshe.
“Kwa nchi zilizoendelea, mapato makubwa ya serikali yanatoka katika mashirika yake kuwapunguzia mzigo maskini wa kulipa kodi ili ziendeshe mashirika hayo, lakini kupunguzia serikali kutegemea kukusanya fedha kutoka kwa watu maskini,” alisema.
Akisisitiza Dk. Mwigulu alisema: “Napendekeza wakuu wote wa mashirika ya umma wafanyiwe usaili kwa ushindani. Napendekeza nafasi zianze kutangazwa punde nafasi ikiwa wazi, ili wenye sifa wajitokeze na wafanyiwe usaili na iwe hivyo kwa bodi. Wenye sifa ndio wafanyiwe upekuzi kufanyiwa uteuzi na kupewa mkataba wenye malengo yanayopimika.”
Dk. Mwigulu alisema mashirika na taasisi, bodi na menejimenti zimezidisha urafi ki unaosababisha wanaendesha ofi si kirafi ki, hivyo hakuna uwajibikaji wa kutosha na kukiuka misingi ya mashirika kuwa na bodi za wakurugenzi.
ADA KIDATO CHA TANO, SITA KUFUTWA
Ili kuwapunguzia gharama, wazazi na wanafunzi kama ambavyo Rais Samia alielekeza, serikali imependekeza kufuta ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ambapo elimu bila ada, itaanza kuanzia shule za msingi hadi kidato cha sita.
Alisema kwa sasa wanafunzi wa kidato cha tano ni 90,825 na kidato cha sita ni 56,880, hivyo mahitaji ya fedha ni kuwahudumia ni sh. bilioni 10.3.
“Serikali imeendelea kugharamia programu ya elimu msingi bila ada ambapo hadi Aprili mwaka huu, sh. bilioni 244.5 zilitolewa. Rais Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, ameguswa na watoto kukatisha masomo kwa ajili ya sababu mbalimbali,” alisema.
Aliongeza: “Miongoni mwa sababu zinazosababisha kukatisha masomo ni umaskini wa kipato katika familia zetu, mimba za utotoni, mwamko duni wa elimu kwa baadhi ya jamii na utoro na wale wasioendelea kufuatana kwa mujibu wa sheria.”
Kadhalika, alieleza serikali imewezesha ujenzi wa madarasa 15,000 katika shule za sekondari, vituo shikizi na mabweni 50 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Ili kukabiliana na utoro wa wanafunzi wanaotoka familia maskini, alisema bado kuna watoto wanaoshindwa kumudu mahitaji ya lazima licha ya kuwepo kwa programu ya elimu bila malipo, hivyo wanasaidiwa na wabunge, madiwani na wengine kuchangiwa na wasamaria wema.
“Napendekeza kuanzisha dirisha maalumu kupitia TASAF itakayosaidia watoto wanaotokea familia maskini.
Kwa msingi huo napendekeza kuanza na sh. bilioni nane kwa watoto masikini watakaopatikana kwenye mfumo wa taarifa za TASAF, taarifa za wabunge na madiwani. Dk. Mwigulu alisema ili kukabiliana na mimba za utotoni, serikali itaendelea kujenga mabweni katika maeneo hatari kwa watoto wa kike.
Aidha, alisema katika kutoa fursa kwa watoto wasioendelea na vidato na vyuo, serikali itaendelea kuimarisha elimu ya ufundi hususan katika vyuo vya kati kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.
CHAGUO NAMBA MOJA MATUMIZI YA TEHAMA
Waziri Mwigulu alisema katika mwaka ujao wa fedha, serikali inapendekeza matumizi ya mifumo ya TEHAMA iwe chaguo namba moja katika utekelezaji wa shughuli za serikali ili kubana matumizi.
Aliagiza kuanzia mwaka ujao wa fedha, ofi si za serikali zianze ‘paperless operations’ (kupunguza matumizi ya karatasi) katika shughuli zake badala yake shughuli zifanyike kwa mtandao, kama ambavyo Bunge limefanikiwa.
“Kumbi za Mikoa na Wilaya zote ziwe na miundombinu ya mikutano ya njia ya Mtandao (Virtual Meeting). Hata wabunge mtaweza kushiriki vikao vya Mabaraza ya Madiwani mkiwa Dodoma au hata nje ya nchi.
“Utaratibu wa kuitana wakuu wa mikoa nchi nzima, wakuu wa idara, wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri na magari kwa nchi nzima na umbali wote kuja kukaa mahali na kusikiliza, ni mzigo kwa walipa kodi,” alisema.
MFUMO WA UNUNUZI KUPITIWA UPYA
Waziri huyo, alisema kuhusu ufanisi katika miradi ya maendeleo, Rais Samia ameelekeza kuangalia upya utaratibu wa ununuzi na thamani ya fedha katika miradi ya maendeleo.
Alisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilionesha bado kuna dosari katika matumizi ya serikali hususani katika ununuzi mkubwa na miradi ya maendeleo.
Waziri Dk. Mwigulu alisema serikali imefuatilia eneo hili na kugundua mfumo wa kufanya ukaguzi wa taratibu za ununuzi (Compliance Audit) na wa kifedha (Financial Audit) ina upungufu.
“Yapo mazingira ya taratibu zote kufuatwa katika ununuzi, sheria zote za ununuzi kufuatwa, na hatua zote za ukaguzi kufuatwa lakini fedha ya umma kuibiwa. Hii inatokana na baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu kupanga njama na wafanyabiashara wasio wazalendo kupandisha bei za bidhaa kwenye zabuni na kujipangia,” alisema.
BAJETI YA KILIMO YAPAA
Kuhusu Kilimo, Waziri Mwigulu alisema serikali imeongeza bajeti ya Kilimo kutoka sh. bilioni 294 hadi sh. bilioni 954 na itaendelea kuongezeka kila mwaka.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kwa zaidi ya asilimia 10 ifi kapo mwaka 2030. Waziri Mwigulu alisema, Bajeti ya mwaka 2022/23 ni msingi muhimu kufi kia lengo hilo kuu pamoja na malengo mengine yakiwemo kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula ndani ya nchi na kuuza nje ya nchi.
Alisema malengo mengine ya uamuzi huo ni kuongeza thamani ya mauzo ya mazao nje ya nchi kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 hadi zaidi ya dola za Marekani bilioni 5 ifi kapo mwaka 2030 ili kuongeza uhimilivu wa deni la Taifa.
“Serikali inakusudia kuongeza mauzo ya Mazao ya Bustani (Horticulture) kutoka dola za Marekani milioni 750 kwa mwaka hadi dola za Marekani bilioni 2 mwaka 2030.
“Ili kupunguza umaskini kwa Watanzania, Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inalenga kutengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya milioni 3 katika sekta ya kilimo ifi kapo mwaka 2025,” alisisitiza.
Alisema hatua hiyo itafanyika kwa kuongeza eneo la umwagiliaji kufi kia hekta 8,500,000 sawa na asilimia 50 ya eneo lote linalolimwa nchini ifi kapo 2030, ambapo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itatekeleza skimu ndogo za umwagiliaji kote nchini.
“Tunataka vijana watoke mjini kuelekea kwenye mashamba ya umwagiliaji kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya kuvunia maji ya mvua.
“Tuna Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na mito mikubwa, kama Malagarasi, Ruvuma, Rufi ji, Mara, Pangani, Ruvu na kadhalika, haya maji tutayatumia kwenye skimu za Umwagiliaji.
“Kwa ardhi, maji na watu tulio nao, ni jambo la aibu kwa Tanzania kulia shida ya ngano, shida ya mafuta ya kula kwa sababu ya vita vya Ukraine na Russia, sisi tunayo fursa ya kuilisha Afrika, Ulaya na Asia katika baadhi ya mazao,” alisema Waziri Mwigulu.
Vilevile, alisema Serikali inakusudia kuongeza idadi ya mashamba makubwa (Block Farms/Commercial Farms) kutoka 110 mwaka 2020 hadi 10,000 mwaka 2030 na kufanya mwelekeo wa uzalishaji wa kilimo kuwa cha kibiashara.
Kwa kilimo cha michikichi, alisema Watanzania waache kung’ang’ania mchikichi mmoja mmoja kila familia na kwamba Mkoa wa Kigoma ndio kitovu cha Michikichi, hivyo upanuzi wa zao hilo utafuata mikoa ya Tabora, Katavi, Pwani, Geita na Kagera.
Alisema wakulima wawezeshwe kuunganisha mashamba ili yawe mashamba makubwa (plantations), kwamba kila mmoja anakuwa mmiliki ili itengenezwe miundombinu ya pamoja yenye dhamira ya kuitikisa dunia.
Dk. Mwigulu alisema kwa alizeti, Serikali inatarajia kufanya tathmini ya kupunguza au kuhamisha mifugo michache iliyopo katika ranchi ya Kongwa ili hekta karibu elfu 38 zitumike kwa kilimo cha alizeti na kiwanda kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki.
Aidha, alisema eneo la Mtanana ambapo huwa Serikali inasumbuka kuweka madaraja pindi maji yanapokata barabara nyakati za mvua, serikali inapanga kuweka Bwawa kubwa ili bonde lote liwe la ‘outgrowers’ wa alizeti.
MKAGUZI WA NDANI APEWA MAJUKUMU
Serikali imemtaka Mkaguzi Mkuu wa Ndani kufanya ukaguzi wa mifumo ili kupunguza uwezekano wa upotevu wa fedha kupitia mifumo ya ukusanyaji na kuepuka matumizi mabaya ya fedha za umma.
Pia, itahakikisha Sheria ya Fedha za Umma, sura 348 inatekelezwa ipasavyo na itakapotokea sheria zimekiukwa, ikiwemo kushindwa kujibu hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ofi sa Masuuli wa Fungu husika atachukuliwa hatua.
Dk. Mwingulu alisema kuna wakati miradi inakamilika na kutumia fedha nyingi lakini miradi inakuwa chini ya kiwango.
“Mheshimiwa Spika, kuna wakati inatokea tunaona miradi ikikamilika, fedha zote zikiwa zimetumika, lakini miradi ikiwa chini ya viwango, jengo au mradi unakamilika ungali bado unanukia rangi lakini ukiwa umetapakaa nyufa kila kona, saruji na tofali zikiwa ni mchanga,” alisema
Aidha, Dk. Mwigulu alisema baadhi ya hatua nyingine zitakazo chukuliwa kwa maofi sa masuuli watakaoenda kinyume ni kuwakata mshahara kati ya asilimia tano hadi 30 kwa mwezi kulingana na uzito wa kosa waliloshiriki kulitenda.
Pia, aliongeza kuwa adhabu nyingine ni kuvuliwa wadhifa alionao au kuondolewa dhamana ya kuwa Afi sa Masuuli wa fedha za fungu husika.
Alisema Rais Samia anakerwa sana na udhaifu uliopo katika eneo la Ufuatiliaji na Tathimini ambapo alisema serikali imetoa mwongozo wa ufuatiliaji na inaandaa sera na baadae itakuja sheria yake.
“Hili litaongezewa rasilimali watu na fedha, litapewa malengo yanayopimika, pamoja na hayo, napendekeza kuanzia mwaka ujao wa fedha taarifa za M&E ziwasilishwe kwenye Baraza la Kazi chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu,” alisema.
Aidha Dk. Mwigulu, alisema katika mwaka wa fedha ujao serikali itaendelea kuimarisha ukaguzi wa ndani ili kuzuia vitendo vya rushwa vinavyofanywa na watumishi wasio waadilifu katika utekelezaji wa miradi.
“Vitendo vya rushwa vinasababisha utekelezaji wa miradi kuwa chini ya viwango, kwa kuwa fedha zilizopangwa kwenda kwenye mradi mingine zinachepushwa na kwenda kwenye mikono ya watumishi wasio wazalendo,” alisema.
Alisema Rais Samia amelikemea vikali suala la rushwa na watu wanaopanga kujinufaisha kupitia fedha za miradi.
“Watu wanapanga kuanzia wakati wa maandalizi ya bajeti, wanafuatilia mchakato wote, siku ikipitishwa na Bunge wanakesha wakishangilia bajeti yao imepita, mradi unaposainiwa wanaanza kugawana fedha kabla ya utekelezaji wa mradi,” alisema.
Alieleza kuwa serikali haitawanyima fedha wananchi wa halmashauri yoyote kwa sababu ya hati chafu na haitarudisha fedha kwenye Mfuko Mkuu kwa sababu hazijatumika kutokana na sababu za uzembe wa baadhi ya watumishi wa umma.
“Wananchi hawahusiki na hati chafu,tutawabaini wazembe, tutawakamata, tutawashitaki na tutawafunga,” alisema.
MARUMARU, MABATI YA NJE YA NCHI YAGUSWA
Pia, Dk. Mwigulu alisema mapendekezo ya mawaziri wa fedha Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) kufanya marekebisho katika viwango vya pamoja vya ushuru wa forodha yanahusisha hatua mpya na zinazoendelea ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2021/22.
Alitaja mapendekezo hayo kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 au dola 1.5 kwa kila mita moja ya mraba kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwa mwaka mmoja katika bidhaa za marumaru.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kulinda viwanda vya ndani vinavyozalisha marumaru na kudhibiti udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo kutoka nje.
Pia, kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 au dola 125 kwa kila tani moja kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa katika mabati kwa mwaka mmoja badala ya ushuru wa asilimia 10 pekee.
“Lengo la hatua hii ni kulinda viwanda vya ndani kutokana na udanganyifu wa thamani halisi ya bidhaa hizo zinapoingizwa kutoka nje, kulinda ajira na mapato ya serikali,” alieleza.
NAFUU MAFUTA YA KULA
Dk. Mwigulu alisema imeondoa ushuru wa forodha wa kiwango cha asilimia sifuri kutoka kiwango kilichokuwa kinatumika cha asilimia 25 kwenye mafuta ghafi ya kula.
Alieleza kuwa lengo la hatua hiyo ni kutoa unafuu kwa wachakataji wa mafuta ghafi nchini ili wananchi waweze kupata mafuta ya kula kwa bei nafuu.
Kadhalika, alisema serikali inapendekeza kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka kutoka kiwango cha awali cha asilimia sifuri kwenye mafuta ghafi ya soya, karanga, nazi na haradali.
“Lengo la hatua hiyo ni kuoanisha viwango vya mafuta hayo ghafi vifanane na viwango vya mafuta ghafi ya alizeti, pamba na mafuta ghafi mengineyo ambayo viwango vyake ni asilimia 10.
Aidha, hatua hiyo inalenga kulinda na kuhamasisha uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kula nchini, kuongeza ajira na kulinda fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta hayo nje ya nchi,” alibainisha.
Pia, alipendekeza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 au dola 500 kwa kila tani moja ya ujazo kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa badala ya asilimia 35 kwa mwaka kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwango cha kati na cha mwisho. Alisema lengo la hatua hiyo ni kulinda viwanda na kuhamasisha uchakataji wa mbegu na mafuta ghafi yaliyoingizwa nchini ili kuongeza thamani ya bidhaa na kukuza ajira.
MILANGO YA ALUMINIAMU NJE YA NCHI BEI JUU
Alisema nchi wanachama wa EAC zimekubaliana kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 kwenye milango na madirisha ya aluminiamu na chuma yanayoagizwa kutoka nje.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kulinda wajasiriamali wa ndani wanaotengeneza bidhaa hizo, kuongeza ajira na mapato ya serikali.
BEI YA SUKARI KUSHUKA
Waziri huyo wa fedha alisema serikali inapendekeza kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya kiwango cha asilimia 100 au dola 460 kwa kila tani moja ya ujazo kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa kwa mwaka mmoja katika sukari ya matumizi ya kawaida inayoagizwa kutoka nje ya wazalishaji wa mbolea lengo la hatua hiyo ni kuleta unafuu kwa wakulima hasa katika kipindi hiki cha mdororo wa uchumi duniani.
Pia, alisema serikali inapendekeza kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye malighafi za kutengeneza mbolea na mashine za kutengeneza mbolea.
VIFAA VYA MACHINJIO
Katika bajeti hiyo, Dk. Nchemba alisema serikali imelenga kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye vifaa vya machinjio hatua ambayo inalenga kuhamasisha ukuaji wa sekta ya mifugo, kuongeza ubora wa nyama, ngozi na kuhakikisha viwanda vya ndani vinapata malighafi za kutosha.
Dk. Mwigului alipendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura 148 ikiwemo kutoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye miti ambayo haijachakatwa.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuchochea ukuaji wa sekta ya misitu, kuongeza ajira na kuwa na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu.
Dk. Mwigulu alieleza kuwa hatua hiyo itapunguza mapato ya serikali kwa kiasi cha sh. bilioni 8.8 ambapo mapato yatakayoongezeka kutokana na ukuaji wa sekta ya misitu na mnyororo wake wa thamani ni sh. bilioni 16.1, hivyo kuleta ongezeko katika sekta hiyo kwa kiwango cha sh. bilioni 7.3.
Pia, alisema serikali imesamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye malighafi zinazotumika kuzalisha mitungi ya gesi, lengo la hatua hiyo ni kuwapa unafuu wazalishaji wa mitungi ya gesi na kulinda viwanda vya ndani.
NEEMA YATUA KWA MACHINGA
Katika bajeti hiyo, serikali imepanga kutenga sh. bilioni 45 kwa ajili ya mtaji kwa wamachinga na kuendeleza ujenzi wa miundombinu kila mkoa.
Pia, Waziri Mwigulu alipendekeza kufanya mgao mpya wa mapato ya asilima 10 ya halmashauri ambapo asilimia tano iwe kwa ajili ya miundombinu na masoko ya machinga, mbili kwa vijana, mbili kwa wanawake na asilimia moja kwa wenye ulemavu.
“Serikali imetenga sh. bilioni 45 kuendeleza ujenzi wa miundombinu na mtaji kwa machinga ambapo kila mkoa, machinga walioko kwenye maeneo yaliyopangwa wawe na ‘revolving fund’ ya sh. bilioni moja kwa utaratibu utakaowekwa,” alisema.
Pia, Dk. Mwigulu alisema serikali itaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wajasiriamali wadogo wanaboreshewa mazingira ya kufanyia biashara, ikiwemo kuwaunganisha na taasisi za fedha ili wapate mikopo nafuu.
Alisema Rais Samia ameahidi kutoa sh. milioni 10 kila mkoa kuimarisha uongozi wa machinga pamoja na ujenzi wa ofi si za machinga.
Aliongeza kuwa serikali imepanga kuweka mazingira rafi ki ya kisheria na kikanuni ili kuharakisha usajili wa biashara, kwa kuhakikisha unakamilika ndani ya siku moja iwapo mwombaji amekidhi masharti yanayohitajika.
Vilivile, alisema serikali inatarajia kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa biashara zinazorasimishwa, kuongeza upatikanaji wa huduma ya miundominu ya biashara, mafunzo teknolojia na masoko.
USAILI KWA KISWAHILI
Katika kuongeza wigo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili serikalini, alisema serikali inapendekeza usaili wote ufanyike kwa lugha hiyo na kumbi zote za mikutano na ofi si za serikali ziwe na vifaa vya kutafsiria lugha za kigeni ili kuienzi lugha ya taifa.
“Hii ndiyo lugha yetu, kwa nini usaili wa mtoto wa Kitanzania anapotafuta kazi unafanyika kwa lugha ya Kingereza? yaani afi sa kilimo, afi sa mifugo, mtumishi wa serikali anakazi ya kuhudumia Watanzania tunapima akili zake kwa kupima Kingereza chake,” alisema.
Dk. Mwigulu aliongeza kuwa Kiswahili ni lugha ya Afrika Mashariki na imepokelewa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU).
Vilevile, aliongeza kuwa UNESCO wameitambua lugha ya kiswahili na watakuwa wanaiadhimisha kila ifi kapo Julai 7 kila mwaka.
“Lugha ya kiswahili ndio lugha ya taifa, ndio lugha ya ofi sini, ndio lugha ya pili kwa watoto wa vijijini na lugha ya kwanza kwa watoto waliowengi wa sasa, ndio lugha ya msingi, ni lugha ya Bunge, na nikiwa Waziri wa Katiba na Sheria nilileta mapendekezo kuifanya kuwa lugha ya Mahakama na lugha ya hukumu,” alisema.
Na WAANDISHI WETU Dar na Dodoma