BENKI ya Dunia (WB), imetoa sh. bilioni 37 za ujenzi wa tawi la Chuo cha Ufundi cha Arusha (ATC), wilayani Hai mkoani, Kilimanjaro, ambacho kitaitwa Kikuletwa, mahususi kufundisha watalaamu wa sekta ya umeme na kuwaongezea ujuzi waliopo kazini.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dk. Musa Chacha, wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kakaigai, katika eneo la Kikuletwa ambako kitajengwa chuo hicho, wilayani humo.
Amesema lengo la ujenzi huo ni kuongeza ufanisi wa kuzalisha watalaamu watakaofanya kazi katika bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji, mkoani Pwani na maeneo yote nchini yanayozalisha umeme.
“Mkuu wa Mkoa, baada ya kupata kiasi hiki cha fedha kutoka serikalini kupitia Benki ya Dunia tumejipanga kuhakikisha tunazalisha wataalamu wazuri wa fani ya umeme.”
“Kuwajengea uwezo wataalamu walioko kazini kwa kuwafundisha kozi za muda mfupi na mrefu ili wakidhi mahitaji ya kuhudumia Bwawa la Mwalimu Nyerere na vyanzo vyote vinavyozalisha umeme nchini ili nchi iwe na umeme wa uhakika muda wote,”alisema.
Mkuu wa Mkoa huo, Kagaigai aliishukuru serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuweka katika Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025 mikakati ya kuboresha sekta ya umeme nchini.
Alisema serikali ina miradi mikubwa ya kuzalisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini na chuo hicho ndicho kinachotegemewa, hivyo waweke mikakati mahususi ya kuisaidia serikali katika sekta ya umeme.
“Nimejulishwa hapa chuo hiki kitakuwa ni mahususi ya kuzalisha wataalamu wa umeme kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika ya Kati.Naomba tengenezeni mikakati mahususi ya kuisaidia serikali. Ili mfanikiwe msikubali kutumiwa na wanasiasa kwa namna yoyote ile katika chuo hiki,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, kuanzia sasa eneo hilo linalindwa kikamilifu kutokana na ubora wake, kama ambavyo madhari yake yanaonekana ya kijani na yenye maji ya kutosha na ya kuvutia.
“Na sisi kama serikali tunawahakikishia kwamba chuo hiki kitakuwa salama na tutasimamia mtekeleze majukumu yenu bila kubughudhiwa na bila adui kuwaingilia kwa namna yoyote ile,” alisema.
Mkuu wa Mkoa huyo alimwagiza kaimu mkuu wa chuo kuhakikisha wanapata hati miliki ya eneo hilo ndani ya miezi mitatu kwa kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Hai.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa utekelezaji wa mradi huo, Dk. Erick Mgaya, alisema fedha zipo tayari na mhandisi mshauri yupo kazini na wameshatangaza zabuni zote muhimu ikiwemo ya vifaa na mradi huo utaanza mapema Mei, mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Juni, mwakani.
Alisema ujenzi huo utajumuisha mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600, maabara tatu kubwa za kisasa ikiwemo mahususi ya kujifunza umeme, vyumba vya madarasa, mkataba ya kisasa, jengo la utawala, zahanati, nyumba 12 za wafanyakazi wakiwemo wakufunzi.
Dk.Mgaya alitaja vitu vingine ni kantini ya wakufunzi na wanafunzi na bweni la kisasa lenye uwezo wa kuchukua watu 50 ambalo litakuwa la wataalamu wa umeme wanaosoma kozi za muda mfupi.
“Baada ya miaka mitatu tutakuwa tumeshajenga kituo cha kuzalisha umeme, pia tutazalisha umeme wa jua na umeme wa upepo, tutakaouuza katika gridi ya Taifa, lengo likiwa ni kuisaidia serikali kuondokana na changamoto ya umeme nchini,” alisema.
NA LILIAN JOEL, HAI



























