TANZANIA na Benki ya Dunia (WB), zimetia saini mikataba miwili ya mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 650 (sawa na sh. trilioni 1.5) kugharamia utekelezaji wa mradi wa kuboresha elimu ya msingi (BOOST) na kuimarisha usalama wa umiliki wa ardhi nchini.
Mikataba hiyo imesainiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na Mkurugenzi wa WB nchini, Mara Warwick.
Akizungumza baada ya kuweka saini mikataba hiyo, jijini Dar es Salaam, Tutuba amesema katika fedha hizo dola za Marekani milioni 150 zitaimarisha usalama wa miliki za ardhi na dola za Marekani milioni 500 zitaboresha elimu msingi.
Ameeleza fedha hizo zilizotolewa na WB ni kupitia mgao wa masharti nafuu wa mzunguko wa IDA 19, akisema miradi iliyo chini ya mikataba iliyosainiwa inatekeleza Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26).
“Fedha hizo pia ni sehemu ya ajenda kuu ya serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inayolenga kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu kupitia mikakati mbalimbali,” alisema.
Alifafanua katika sekta ya elimu ya msingi, fedha hizo zitatumika kuboresha na kusimamia mazingira shirikishi ya kufundishia na kujifunzia, uwezo wa walimu, kukuza na kuhamasisha matumizi ya TEHAMA katika shule za awali na msingi.
“Mradi wa BOOST unakusudia kuboresha usawa katika upatikanaji wa elimu bora ya awali na msingi kwa upande wa Tanzania Bara ukiwemo ujenzi wa vyumba 12,000 vya madarasa na vifaa vinavyohitajika vya elimu.
“Usimikaji wa mifumo na usambazaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule na vyuo vya ualimu 800 kwa pamoja na kuongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za awali na msingi,” alisema.
Aliongeza katika sekta ya ardhi, kazi zitakazofanyika ni kukuza na kuwezesha upangaji, upimaji na utoaji hatimiliki za ardhi kwa ajili ya uwekezaji na usalama wa makazi ya watu.
Alitaja mambo mengine ni kuboresha na kuongeza mfumo unganishi wa taarifa za usimamizi wa ardhi na kukuza matumizi ya TEHAMA katika upimaji na uandaaji wa hatimiliki ya ardhi.
“Mradi huu unatarajia kunufaisha nchi kupitia ongezeko la usalama wa umiliki katika wilaya 40 zilizochaguliwa, kwa kutoa hati za kimila (CCROs), hati za kumiliki ardhi mijini (CROs) na leseni za makazi. Aidha, mradi utaongeza ufanisi wa usimamizi wa taarifa za ardhi kupitia uboreshaji wa Mfumo wa Kidijitali wa Taarifa za Ardhi (ILMIS) na utengenezaji wa ramani za msingi (Base Maps),” alifafanua.
Tutuba alisema kusainiwa mikataba hiyo, kumefanya kiwango fedha kilichowekezwa na WB nchini kufikia dola za Marekani bilioni 6.15 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Aidha, aliwaagiza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Allan Kijazi na Katibu MKuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Eliamani Sedoyeka wasimamie ukamilishaji wa masharti yote ya awali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia nchini, Mara Warwick, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu na kwamba fedha zilizotolewa zitawanufaisha zaidi ya wanafunzi 12,000 wanaosoma masomo ya awali na elimu ya msingi.
Aliongeza kwamba WB pia, imeidhinisha mkopo wa dola za Marekani milioni 150 kwa sababu mpango wa kuimarisha masuala ya ardhi utawanufaisha zaidi ya wananchi milioni mbili hususan wanaoishi vijijini kwa kupatiwa hatimiliki za kimila zaidi ya 500,000 katika Mikoa 14 yenye Wilaya 40.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Allan Kijazi alisema fedha hizo hasa zilizoelekezwa katika ardhi, zitatumika kusimika mifumo ya kielektroniki katika mikoa 24 kwa kujenga ofisi za ardhi na kufanya ufuatiliaji na tathimini ya mradi.
WACHUMI
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Razack Lokina, alisema fedha hizo ni matokeo ya juhudi za Rais Samia hasa kujenga uhusiano mwema na nchi washirika na jumuiya za kimataifa.
Alifafanua huo ni mkopo wa masharti nafuu kwa maana ni fedha ambayo haiipi nchi mzigo wakati wa kurudisha, badala yake zinaharakisha utekelezwaji wa miradi iliyokusudiwa.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Tawi la Mizengo Pinda, Katavi, Profesa Anna Sikira, alisema uhusiano mzuri baina ya mataifa yanajenga diplomasia imara miongoni mwa mataifa hayo.
Alieleza kwa sasa Tanzania inasomeka kimataifa na matunda yake ndiyo yanayoonekana sasa, hivyo wananchi watarajie kuona makubwa zaidi.
Profesa Anna alisisitiza umuhumi wa kuendelezwa usimamizi wa fedha hizo ili zitumike katika shughuli lengwa.
Na MWANDISHI WETU



























