Na MUSSA YUSUPH
BUNGE limeelezwa kwamba Tanzania inatumia wastani wa sh. bilioni 474 kwa mwaka katika kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.
Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM), Assa Makanika.
Mbunge huyo aliuliza kwanini serikali haioni umuhimu wa kuwekeza yenyewe katika zao la mchikichi badala ya kuziachia halmashauri ili kukabiliana na upungufu wa mafuta nchini.
Akijibu swali hilo, Bashe alisema katika kipindi cha mwaka 2019/20 hadi mwaka 2020/2021, serikali imewekeza sh. 5,820,361,798 kwa ajili ya kuendeleza zao la chikichi.
Alisema hadi kufikia Januari 31, mwaka huu, miche bora ya michikichi 2,244,935 imezalishwa na jumla ya miche 1,456,111 ilisambazwa kwa wakulima katika halmashauri za wilaya za mkoa wa Kigoma na miche 788,824 inatarajiwa kusambazwa kwa wakulima katika msimu wa 2020/2021.
Kadhalika, Bashe alieleza katika mwaka 2021/2022, serikali imetenga jumla ya sh. 3,158,200,000 kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza mbegu na miche ya zao la michikichi.
“Mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa tani 570,000 kwa mwaka. Hata hivyo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufikiwa wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka, ambapo husababisha nchi kutumia wastani wa kiasi cha sh. bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka,” alieleza.
Naibu waziri huyo alisema kama ilivyo kwa mazao mengine, serikali huwekeza katika utafiti, uzalishaji na upatikanaji wa pembejeo za kilimo, huduma za ugani, udhibiti wa visumbufu vya mazao na utafutaji wa masoko.
Alisema katika utekelezaji mikakati hiyo, serikali imekuwa ikishirikiana wadau mbalimbali zikiwemo mamlaka za serikali za mitaa na sekta binafsi.
Bashe alieleza kama sehemu ya mkakati wa kujitosheleza kwa mafuta ya kula, mwaka 2018 serikali iliamua kuanzisha kituo maalum cha utafiti wa zao la michikichi cha TARI Kihinga mkoani Kigoma ili kuendeleza zao hili kwa ufanisi zaidi.
“TARI Kihinga inashirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), halmashauri na sekta binafsi katika utafiti, uzalishaji wa miche bora ya michikichi na kuisambaza kwa wakulima. Serikali itaendelea kushirikisha wadau wa sekta ya umma na binafsi kuendeleza zao la mchikichi na mazao mengine ya mbegu za ili kuwezesha nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kula.
“Mamlaka za Serikali za Mitaa zinashauriwa kuwekeza katika mazao ya kilimo kutokana na mapato yatokanayo na ushuru wa mazao ikiwemo zao la michikichi,” alibainisha.



























