BONDIA wa kulipwa wa Tanzania, Zulfa Macho, ameiomba serikali kupitia mashindano ya michezo kwa shule za msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) kuanzisha mchezo wa ngumi ili kuibua vipaji vya mchezo huo.
Akizungumza Dar es Salaam na Uhuru Online, Zulfa amesema kuwepo kwa mchezo huo shuleni kutasaidia kukuza na kuendeleza vipaji nchini.
Zulfa ameeleza kuwa mchezo wa ndondi unapaswa kuwekewa misingi imara kuanzia ngazi ya chini kunakopatikana vijana wenye damu changa
“Mimi nashauri kuwepo kwa mchezo wa ngumi shuleni itachangia kukuza vipaji, mfano katika soka tunawawakilishi wazuri ambao wanapeperusha vema bendera ya taifa,” amesema.
Bondia huyo ameongezea kuwa mchezo huo sasa unapaswa kupewa nafasi ili taifa lipate mabondia ambao watatangaza taifa katika anga za kimataifa, maradufu ya ilivyo sasa.
“Kuna mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA, mchezo huu ukiwekwa shuleni itachangia kupata mabondia wengi na kuinua vipaji vya vijana, kuna watoto wengi mtaani ambao wana ndoto za kuwa mabondia wakubwa,” amesema.
Zulfa ambaye ameshinda mapambano mbalimbali, likiwemo pambano la mkanda wa ubingwa wa UBO, alipomchakaza Halima Vunjabei kwa pointi pambano lililofanyika katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam Aprili 11, mwaka huu.
Na Amina Kasheba