BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imeandaa mikakati minne, kudhibiti vitendo vya kukosekana uadilifu miongoni mwa watumishi wa sekta ya benki nchini, ambao wamekuwa chanzo cha matatizo.
Matatizo hayo ni ongezeko la mikopo isiyolipika muda mrefu ‘chechefu’ katika sekta ya benki, hivyo kuzilazimu benki na taasisi za fedha kutoza viwango vikubwa vya riba za mikopo kwa wateja wake.
Gavana wa BoT, Florens Luoga, ameeleza kupitia taarifa yake kwa umma kuwa, mikakati hiyo ina lengo la kumaliza changamoto hiyo, ambayo inachangiwa na uwepo wa baadhi ya watumishi wa benki wasiokuwa waadilifu kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, BoT imefanya utafiti katika sekta ya benki na kubaini kukosekana uadilifu kumechangia kutolewa kwa mikopo bila kuzingatia utaratibu, hivyo kuzalisha tatizo la mikopo chechefu.
Profesa Luoga amesema katika taarifa hiyo kuwa, hali hiyo inahatarisha uimara wa sekta ya benki na kuathiri uchumi wa nchi.
Ameutaja mkakati wa kwanza ni kuendelea kufanya ukaguzi wa benki na taasisi za fedha ili kubaini sababu za kuongezeka mikopo chechefu na wafanyakazi ambao wanahusika moja kwa moja na kadhia hiyo.
“Iwapo itathibitika kuna mfanyakazi wa benki anahusika katika kutoa mikopo bila kuzingatia taratibu, kukosa uadilifu na kushirikiana na wakopaji katika kutoa mikopo kiuhalifu na vitendo vya rushwa
“Benki au taasisi ya fedha husika itatakiwa kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya mfanyakazi huyo na BoT itamfungia mfanyakazi huyo kuajiriwa na benki au taasisi yoyote ya fedha inayoendesha shughuli zake nchini,” imeelezwa katika taarifa hiyo.
Mkakati wa pili, BoT imezitaka benki na taasisi za fedha ambazo wafanyakazi wake wana mikopo chechefu katika benki au taasisi za fedha nyingine, kuwasilisha taarifa zao katika taasisi za kuchakata taarifa za mikopo (credit reference bureau).
Hatua itakayofuata, BoT itawazuia wafanyakazi husika kupata ajira katika benki au taasisi yoyote ya fedha inayoisimamia, endapo itabainika kushindwa kwao kurejesha mikopo kumetokana na uzembe, uhalifu au kukosa uadilifu.
Mkakati wa tatu, BoT imezitaka benki na taasisi za fedha kutokutoa mikopo kwa wakopaji wasiokuwa waaminifu au ambao wanakopa kwa kutumia njia za udanganyifu na kuacha kulipa.
Imesema taarifa za wakopaji wa aina hiyo, zitatunzwa katika rejesta maalumu na benki na taasisi za fedha zitapewa orodha yao kwa lengo la kuhakikisha kuwa hawapati mikopo katika sekta ya benki.
“Kwa sasa, wakopaji wa aina hii wanapewa muda wa miezi mitatu, kuanzia tarehe ya taarifa hii (jana), kufanya mipango ya kurejesha mikopo yao kabla majina yao hayajaingizwa katika rejesta maalumu na benki na taasisi za fedha kupewa orodha hiyo,” alieleza Gavana Luoga.
Kadhalika, mkakati wa nne ni kuziagiza benki na taasisi za fedha kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wa umma ambao wana mikopo chechefu ili hatua stahiki zichukuliwe.
Aidha, ameeleza katika taarifa hiyo kuwa taarifa za wakopaji kama hao pia zitaingizwa katika rejesta maalumu na benki na taasisi za fedha zitapewa orodha yao, ili kuhakikisha hawapati mikopo mingine mpaka hatua stahiki zitakapochukuliwa dhidi yao na wameanza kurejesha mikopo.
“Benki Kuu ya Tanzania inatoa wito kwa wananchi wote ambao wana mikopo kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kurejesha mikopo wanayokopa katika benki na taasisi za fedha,” alisisitiza Gavana.
Aidha, amesema wananchi wanahamasishwa kutoa taarifa katika benki na taasisi za fedha au Benki Kuu kuhusu vitendo vya uhalifu au rushwa wanavyokutana navyo wakati wanapohitaji huduma kutoka katika benki au taasisi ya fedha.
Amesema BoT itaendelea kuwasiliana na benki na taasisi za fedha kuhakikisha taratibu za utoaji mikopo zinazingatiwa kikamilifu kwa lengo la kudhibiti kuongezeka mikopo chechefu.
Kufuatia uamuzi huo wa BoT, mdau mmojawapo wa masuala ya fedha na uchumi nchini, Noel Mmbaga, ambaye ni mmiliki wa taasisi binafsi ya mikopo, aliliambia UhuruOnline kuwa mazingira ya utoaji wa mikopo kutoka baadhi ya benki yamekuwa magumu, hali inayokaribisha mazingira ya rushwa.
Na WILLIAM SHECHAMBO



























