Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. John Magufuli amefariki dunia katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akitangaza kifo cha Rais, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, alisema Dk. Magufuli alifariki dunia jana hospitalini hapo saa 12 jioni, alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Ndugu wananchi, kwa masikitiko makubwa nawajulisha kuwa, leo (jana) tarehe 17, Machi mwaka huu 2021, majira ya saa 12 jioni, tumempoteza kiongozi wetu shupavu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Joseph Magufuli, ambaye amefariki kwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Mheshimiwa Rais Mafuli alilazwa tarehe 6, Machi mwaka huu, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa tatizo la moyo la mfumo wa umeme ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10, aliruhusiwa tarehe 7, Machi mwaka huu na kuendelea na majukumu yake.
“Tarehe 14 Machi mwaka huu, alijisikia vibaya na akakimbizwa Hospitali ya Mzena ambapo aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hadi umauti ulipomkuta. Mipango ya mazishi inafanywa na mtajulishwa.
Nchi yetu itakuwa katika kipindi cha maombolezo kwa siku 14, na bendera zitapepea nusu mlingoti. Bwana ametoa, bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,” alisema Makamu wa Rais Samia wakati akilitangazia taifa msiba huo mzito kupitia televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
HISTORIA YA DK. MAGUFULI
Rais Dk. Magufuli alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1959 katika Wilaya ya Chato ambayo ni mojawapo ya wilaya tano za Mkoa wa Geita.
Wilaya ya Chato ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera na ni mwaka 2012 tu ndipo ilipohamishiwa Mkoa wa Geita.
Magufuli alipata elimu ya msingi katika Shule ya Chato na masomo ya sekondari ya
awali katika Seminari ya Katoke, Biharamulo. Alimalizia kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lake, mkoani Mwanza. Kidato cha sita alimalizia katika sekondari ya Mkwawa mkoani Iringa.
Wasifu wa Magufuli unaonyesha kwamba alipata cheti cha Stashahada ya Ualimu katika Chuo cha Elimu Mkwawa mnamo mwaka 1982 alikojikita zaidi katika masomo ya hisabati na kemia.
0Kati ya mwaka 1985 hadi 1988, Magufuli alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya masomo yake ya shahada ya kwanza ya ualimu wa kemia na hisabati.
Alijipatia shahada yake ya uzamili kwenye kemia kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Salford cha Uingereza kati ya mwaka 1991 na 1994.
Wakati akiwa waziri katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2009, Magufuli alijiunga na UDSM alikosomea Shahada ya Uzamivu katika kemia (PhD-Chemistry).
Magufuli aliingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza mwaka 1995 wakati alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na
hakuwahi kukaa nje ya baraza hilo tangu wakati huo.
Amewahi kuwa waziri katika wizara tofauti kama vile Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mwaka 1995 Dk. Magufuli alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki mkoani Kagera, baadae mwaka 2000 alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa mbunge wa Biharamulo bila ya kupingwa na baadae aliteuliwa kuwa waziri kamili katika Wizara ya Ujenzi.
Magufuli alichaguliwa tena kuliongoza jimbo hilo bila kupingwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na baadae aliteliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Dk. Magufuli alipitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wa kiti cha urais nafasi ambayo alishinda na kuongoza kwa miaka mitano hadi 2020 ulipo fanyika uchaguzi mwingine nao akashinda kwa kishindo.