ILIKUWA saa 4:31 asubuhi ya jana wakati nikiingia ofisini nilipokea simu kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari wa gazeti hili Uhuru, William Shechambo, nikajua anataka kunijulisha hali za wagonjwa wake, maana alikuwa anauguliwa na mkewe na mwanawe.
Kama nilivyohisi kweli alinielezea juu ya hali za wagonjwa wake, huku akiniambia kwamba wanaendelea vizuri na anamshukuru Mungu kwa jinsi wanavyoendelea kuimarika. Basi nami nikamueleza kwamba hayo ndiyo majukumu ya mume kwa mke na mzazi kwa mtoto kwamba lazima uwajibike katika kila changamoto wanazozipitia.
Basi baada ya maelezo yangu kwake, Shechambo alinieleza:”Chief hata hivyo nimepokea taarifa za kustusha kutoka kwa ndugu yake na Zahor, kwamba amefariki dunia,” alisema Shechambo na kufafanua kwamba aliyempigia simu alijitambulisha anaitwa Zahor na ni ndugu wa Rashid Zahor ambaye sasa ni marehemu.
Kwa mujibu wa Shechambo mtoa taarifa (Zahor) alimweleza kwamba aliipata namba yake baada ya kupekua simu ya marehemu na kugundua ndiye mtu aliyekuwa akiwasiliana naye sana kupitia ujumbe mfupi wa maandishi na ndipo alipoamua kumpigia na kumpa taarifa za kifo cha nduguye huyo.
Shechambo alisema Zahor (mtoa taarifa), alimweleza kwamba nduguye (Rashid) alifariki dunia saa tatu asubuhi huko Chanika, nyumbani kwa dada yake kutokana na maradhi ya kisukari na shinikizo la damu, ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Nilistuka na kuingiwa na simanzi kubwa kutokana na ukweli kwamba si muda mrefu niliwasiliana na Zahor, huku akinielezea changamoto za kiafya anazopitia.
Alinieleza jinsi anavyopambana na kisukari na vidonda vya tumbo, nami nikamsisitizia umuhimu wa kuzingatia tiba na masharti ya madaktari.
Hata hivyo, hivi karibuni nilimpigia simu kumjulia hali, lakini simu yake iliita bila kupokelewa, nikatuma ujumbe mfupi wa maandishi nao haukujibiwa. Siku iliyofuata nilimuuliza mfanyakazi mwenzetu Bi Mariam Mkali, ambaye anaishi naye jirani katika nyumba za kampuni zilizoko Tabata Mawenzi, akaniambia ni kweli anaumwa lakini mara nyingi huwa hayupo nyumbani kwake.
Mapema wiki hii, Mpiga Picha wetu Mkuu, Yassin Kayombo akiwa chumba cha habari alisikika akisema Zahor ni mgonjwa na anaugulia kwa ndugu yake mmoja maeneo ya Chanika, hivyo tulimtaka afuatilie na kutujulisha mahali hapo ili tuweze kwenda kumjulia hali.
Ni juzi tu Kayombo alirudi na jibu na kutueleza mahali anapopatikana Zahor, lakini kabla ya kufanyika kwa taratibu za kwenda kumjulia hali, habari za simanzi ndizo zilizotufikia katika hali ya kustukiza na kutuacha na majonzi makubwa.
Zahor ambaye mpaka umauti unamkuta alikuwa ndiye Msanifu Mkuu wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, binafsi nina historia ndefu naye, kwani tuliajiriwa wote katika Shirika la Magazeti ya Chama, tukiwa vijana wadogo baada ya kuhitimu elimu ya sekondari.
Wote tulianzia Dawati la Michezo lakini mwenzangu alikuwa mzuri zaidi katika uandishi wa habari za michezo, hivyo aliendelea kudumu katika dawati hilo, mimi nikihamishwa kwenda Dawati la Habari chini ya Mhariri mkongwe Joe Nakajumo.
Kutokana na uwezo wake, Zahor akiwa bado kijana mdogo mnamo Machi 14, 1997 aliaminiwa na Bodi ya Uhariri ya wakati huo, chini ya uongozi wa Kaimu Mhariri Mkuu Josiah Mufungo, kuwa Kaimu Mhariri wa Habari za Michezo baada ya Godrey Lutego, kuacha kazi.
Miongoni mwa majukumu aliyopewa ni pamoja na kuwa kiongozi wa sehemu ya michezo na kwamba watendaji wote wa sehemu hiyo watawajibika kwake. Barua yake ya uteuzi ilimwelekeza pia atasimamia ukusanyaji wa habari, makala na picha zinazohusu michezo, burudani na sanaa na kuziwasilisha kwa Msanifu Mkuu kwa kuzingatia ‘dead line’ ya wakati huo.
Kimsingi msiba wa Zahor ambaye tulikuwa tukitaniana sana kutokana na ukweli kwamba ni miongoni mwa waandishi wa muda mrefu tuliosalia katika chumba cha habari cha Uhuru na Mzalendo, tulioajiriwa katika miaka 1990 tukiwa vijana wadogo.
Mara nyingi tulikuwa tukitaniana na kuitana majina tofauti tofauti kama vile Zungu, Baharia, Shemeji, vijana wa zamani, doctor na mengine mengi tu, ilihali tulikuwa ni watu tuliofahamiana sana na wenye kuheshimiana inapofika suala la kazi.
Tuliwahi kutaniana kwamba kwa kuwa tunafahamiana sana, basi siku mmoja wetu akiitwa mbele ya haki basi mwenzie amuandikie ‘orbituary’ yaani buriani kwa tafsiri ya haraka haraka na kweli baada ya kupata taarifa za kifo cha ‘Doctor’niliona pamoja na makujumu yangu mengi kwa sasa, lakini nawajibika kuandika hii buriani kumuenzi mwenzangu ambaye nimedumu naye ndani ya chumba cha habari cha Uhuru kwa takriban miaka 28 sasa.
Pamoja na kwamba Zahor hakuwahi kupata mafunzo ya muda mrefu ya tasnia ya uandishi wa habari, lakini uwezo wake wa uandishi ulijengeka siku hadi siku kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo katika fani hiyo, pamoja na usaidizi mkubwa alioupata kutoka kwa Wahariri wakongwe kwenye chumba cha habari cha Uhuru kuanzia pale Pugu Road sasa Nyerere na baadaye Lumumba ambako ndiyo makao makuu ya Uhuru Publications Ltd hadi sasa.
Miongoni mwa Wahariri wakongwe ‘walimpika’ Zahor ‘Ramoza’ ni Marehemu Ahmed Shimye, Masoud Saanani, Lutego kwa upande wa habari za michezo na Nakajumo, Mwadini Hassan na Jacqueline Liana. Wengine ni Said Nguba na Mufungo ambao kwa nyakati tofauti waliongoza kampuni ya Uhuru Publications.
Kutokana na ‘kupikwa’ na Wahariri hao wachache niliowataja Zahor, alichipukia kuwa mwandishi mzuri si kwa habari za michezo, bali hata katika dawati la habari za kawaida na uandishi wa makala.
Ndani ya chumba cha habari waandishi wengi walipenda kumtania kwa kumwita ‘Doctor’ si kwa sababu alikuwa na ufahamu wowote kuhusiana na masuala ya tiba, bali kutokana na uwezo wake wa kumudu madawati yote kiutendaji. Ni miongoni mwa waandishi wa habari wachache wenye uwezo wa kutumika katika madawati yote pasipo kutiliwa shaka.
Binafsi nilipenda kumwita ‘kiraka’ kwani kila upungufu ulipojitokeza katika eneo fulani nilimuomba Zahor asaidie na kazi zilikwenda bila matatizo.
Mfano mzuri ni jinsi alivyoweza kumudu uandaaji wa matoleo maalumu ya shughuli za Chama, ikiwemo mikutano mikuu, kampeni na habari za bunge. Kutoka na uwezo na uzoefu wake, Bodi ya Uhariri haikusita kumpa nafasi ya kuwa Msanifu Mkuu, ambaye kwa utaratibu wa uendeshaji wa vyombo vya habari hususan magazeti ndiye ‘chujio la mwisho’ kabla ya habari au makala kwenda kwa mchapishaji.
Daima tutamkumbuka Zahor kutokana na umakini na uwajibikaji wake anapokuwa kazini, kwani anapokaa katika dawati alikuwa si mtu wa kuzurura au kuongea sana, bali alihakikisha anamaliza kazi yake kwa muda na anapohakikisha gazeti limetumwa kiwandani alikuwa akichukua magazeti na kuondoka.
Alipenda sana sanaa, michezo na burudani hususan muziki wa bendi na hasa nyimbo za zamani zilizoimbwa na kina Marijani Rajab, Mbaraka Mwinshehe na aliwahi kuwa Mshauri wa Bendi ya Sikinde wa masuala ya habari.
MHARIRI CHIFU JOE aeleza alivyomfahamu Zahor
Akiwa kwenye chumba cha habari jana Chief Joe alikuwa miongoni mwa waandishi waliopekea taarifa za kifo cha Zahor na alimwelezea kwamba marehemu Zahor ni Mwandishi wa habari aliyefunzwa na kulelewa na magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Tangu ujana wake hadi umauti ulipomfika jana alikuwa anayatumikia magazeti ya Uhuru na Mzalendo katika vitengo mbalimbali.
Zahor alikuwa na kipaji cha utunzi wa hadithi na ndicho kilichomfanya aungane na magazeti haya.
Alianza kutunga hadithi na kuzileta kuchapishwa katika gazeti la Mzalendo miaka ya 1980 mwishoni wakati huo akiwa mwanafunzi wa shule ya sekondari.
Miongoni mwa hadithi za kusisimua aliita ‘Uliyataka Mwenyewe’. Hadithi hii ilimwelezea kijana aliyemtaja kwa jina la Ramoza jinsi alivyokutana na msichana Anie. Ramoza ni kifupi cha majina yake ambayo ni Rashid Mohammed Zahor.
Hadithi hiyo ilitoka mfululizo katika gazeti la Mzalendo kila Jumapili kuanzia Mzalendo ya Jumapili Februari 7, mwaka 1993 na kumalizia katika Mzalendo ya Jumapili ya Februari 28.
Tangu nilipomfahamu wakati huo, Zahoro ambaye alikuwa ni kijana mtaratibu na mwenye kupenda kujifunza, alikuwa anakuja kwenye ofisi za magazeti barabara ya Pugu, sasa inaitwa Nyerere kuleta hadithi.
Kwa kuwa alikuwa ni mtunzi mzuri wa hadithi za kusisimua na tayari alikuwa ameyafahamu na kuyazoea mazingira ya utendaji kazi ndani ya chumba cha habari, uongozi wa Shirika uliamua kumuajiri. Katika ajira yake mpya alianzia kitengo cha habari za michezo.
Jane Mihanji amlilia Zahor
Zahor alikuwa akiniita dada siku zote, akinipa heshima ya jinsia yangu na ukaribu wetu katika utendaji kazi. Akiwa msanifu mkuu wa magazeti yetu, nilikuwa msaidizi wake. Pamoja na kwamba alikuwa bosi wangu, hakuwai kuleta dharau kutokana na nafasi yake.
Alikuwa ni mtu mcheshi na mara zote akiniona baada ya salaamu lazima ilikuwa achomeke utani wa jambo fulani, tukikumbuka maisha ya zamani ya chumba cha habari na viongozi wetu ambao wengi wamestaafu.
Zahor alikuwa ni mchapakazi na aliipenda kazi yake. Hata nilipokuja kupanda cheo na kuwa Naibu Mhariri katika magazeti yetu, aliona tu kuwa ni sehemu wa mgawanyo wa majukumu. Aliendelea kunipa heshima kama dada yake na kiongozi wake. Nami pia wakati nikiwa na nafasi hiyo, sikuwa nimeacha kuhariri, kwa hiyo mara zote tulikuwa tukikutana kwenye kazi.
Ni mtu aliyekuwa akipenda kujifunza, kwani alianza katika uandishi wa hadithi, lakini kwa vile alikaa muda mwingi na waandishi wa habari, alijikuta akianza kuandika habari za michezo na baadaye ‘hard news’ hadi kuja kupewa majukumu makubwa ya usanifu.
Kwa mujibu wa familia ya marehemu Zahor anatarajiwa kuzikwa leo katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar er Salaam.
Ninachoweza kusema Zahor ameitendea haki fani ya uandishi wa habari, kwani ameshiriki kikamilifu katika kuboresha kazi za uandishi wa habari ndani ya chumba cha habari cha Uhuru, akiwa Mhariri wa Michezo, Mhariri wa Burudani na hatimaye Msanifu Mkuu wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Mwenyezi Mungu awape wepesi ndugu na jamaa wa marehemu Zahor katika kipindi hiki kigumu wanachokipitia kutokana na kifo cha mpendwa wao.
Kwa kheri ‘Doctor’ mwendo umeumaliza kwa kishindo.
Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un
Na Ramadhani Mkoma