Na SALVATORY NTANDU
UKUSANYAJI mbovu wa mapato ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga umetajwa kuchangia kupatikana kwa hati chafu, baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubaini zaidi ya sh. bilioni 1.8 za mapato ya ndani zilizokusanywa hazijaingizwa kwenye mfumo na hazijulikani zilipo.
Kufuatia hali hiyo baraza la madiwani la halmashauri hiyo, liloketi hivi karibuni, limeagiza watumishi na mawakala wa ukusanyaji wa mapato waliohusika na ubadhirifu huo wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kurejesha fedha walizokusanya na kutoziingiza kwenye akauti za halmashauri.
Diwani wa viti maalumu Kata ya Mwamala, Anna Shiloti, amesema kutoingizwa kwa fedha hizo kwenye mfumo kumesababisha CAG kutoridhika na ukusanyanji na usimamizi wa mpato ya halmashauri hiyo, uliotekelezwa na watumishi na mawakala waliopewa zabuni za kukusanya mapato.
“Sisi kama madiwani wa halmashauri hii tumepata aibu haiwezekani tusimamie ukusanyaji wa mapato katika kata zetu lakini baadhi ya watumishi na mawakala wazembe washindwe kuziingiza katika mfumo na kutusababishia kupata hati chafu,tunaiomba serikali iwachukulie hatua kali za kisheria haraka waliohusiaka na ubadhirifu huu,” amesema Shiloti.
Ngassa Mboje, qmbaye ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, amesema ili kujibu hoja zote za ukaguzi zilizoibuliwa na CAG, inapaswa watendaji wote walioshindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu, wawajibishwe na kama kuna fedha wamezitumia kwa manufaa yao binafsi wakatwe mishahara ili kufidia deni hilo ambalo linazidi kukua kila mwaka.
“CAG ameonesha wahasibu wetu wameshindwa kuandaa ripoti za kufunga hesabu za fedha za mwaka kwa ufasaha kama tunawatumishi hawana sifa ni bora wakatupisha,haiwezekani wataalamu wetu waendele kutukwamisha na kusababisha halmashauri yetu kupata hati chafu kwa kufanya kazi kwa mazoea,”amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Hoja Mahiba, amesema tayari maofisa wa Tehama kutoka TAMISEMI wako wanaendelea kuufanyia uhakiki mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekroniki, ili kubaini ukweli wa deni hilo ambalo hapo awali lilikuwa ni shilingi bilioni 2.8 ambapo mpaka sasa limepungua hadi sh. bilioni 1.8.
“Nimekwisha chukua hatua kwa watumishi Zaidi ya 25 waliohusika kuhujumu mfumo wa ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kuwakata mishahara kwa asilimia 15 ili kuhakikisha fedha ambazo waliziiba zinarejeshwa.
“Madeni mengi yanayoonekana kwenye mfumo ni zamani kuanzia mwaka 2016 nadi 2018, ambapo fedha nyingi hazijulikani zilipo,”amesema Mahiba.
Mwakilishi wa CAG mkoani humo, Anselem Tairo, amesema halmashauri hiyo imepata hoja za ukaguzi 87, ambazo wanapaswa kuzijibu ikiwa ni pamoja na kutoandaliwa kwa usahihi kwa taarifa za kifedha, mapato kutowasilishwa benki, uhamisho wa fedha kutoka kwenye akaunti za mapato kwenda kwenye akaunti za matumizi.
Akitoa kauli ya serikali mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk Philemoni Sengati amesema watumishi waliobainika kufanya ubadhirifu wa fedha hizo watachukuliwa hatua kali za kisheria, na kumwagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa na watumishi na mawakala zinaingizwa kwenye akaunti ndani ya saa 24.