KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameutaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kununua mahindi kwa wakati ili kuwafanya wakulima kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Pia, ameitaka NFRA kumwandalia ripoti itakayomwonyesha ni namna gani mahindi ya wakulima yananunuliwa na kuahidi kupita katika vituo vinavyokusanya mahindi hayo.
Kauli hiyo aliitoa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, wakati akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ambapo alisema tayari Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mahindi hayo kwa wakulima kwa awamu ya pili.
Alisema kama Rais Samia ametoa fedha za kununulia mahindi, ni lazima watu wa NFRA wachangamke kwani kazi ya fedha siyo kukaa katika mifuko au akaunti za taasisi, bali kazi yake ni kuelekezwa katika maeneo yaliyokusudiwa.
Chongolo alisema mwananchi amelima shamba lake kwa bidii, kavuna vizuri mazao yake anataka kutengeneza mambo yake na anataka kujipanga na pembejeo za msimu ujao wakicheleweshwa kwenye mambo ya Msingi watakuwa hawatendewi haki.
“Sisi tufanye kazi yetu kwa msingi, tununue mahindi kwa wakati, mahindi yakishanunuliwa mwananchi atajipangia mwenyewe manunuzi yake, kwa sababu fedha ni ya kwake,” alisema.
Alisema Rais Samia amemtuma kujiridhisha kama mahindi yamenunuliwa kwa fedha za awamu ya pili.
“Niliongea na Rais Samia leo (jana) ameniambia ametoa fedha sh. bilioni 50 kwa awamu ya pili ya ununuzi wa mahindi na awamu hii ameongeza fedha, akaniambia nije kujiridhisha kama NFRA wameanza kununua mahindi,” alisema na kuongeza.
“Rais Samia anajua watu wa Mbinga mnalima sana mahindi na kahawa, anajua mnavyohangaikia shughuli mbalimbali za kujikwamua na umasikini, hapa Mbinga najua kuna vituo viwili vya kununulia mahindi, kimoja kipo Mbinga mjini na Kingonsera, pelekeni mahindi yenu serikali inunue,” alisema.
Chongolo aliwaomba wananchi wa Mbinga kulima mazao mengine ambayo yanastahimili katika eneo la mkoa huo, ili kuendeleza, kupanua wigo wa mzunguko wa kipato.
Na MWANDISHI WETU





























