KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema CCM itaendelea kuwa chama imara cha siasa Afrika, kama ambavyo hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyokuwa akisisitiza.
Amesema katika kuadhimisha miaka 22 tangu kufariki dunia kwa Mwalimu Nyerere, CCM itaendelea kuenzi mchango wa Baba wa taifa kusisitiza siasa safi na uongozi bora.
Akihojiwa na UhuruOnline, Shaka amesema Mwalimu Nyerere ameacha funzo kubwa kwa viongozi, hususan ujasiri katika kufikia uamuzi na ustahimilivu wa kisiasa.
“Mwalimu Nyerere alikuwa kielelezo ambacho kumbukumbu za nchi yetu zinatuambia wakati ule, kulikuwa na watu ambao hawakuamini kuwa anaweza kung’atuka na wapo ambao hawakutaka Mwalimu Nyerere ang’atuke kutokana na kazi nzuri aliyoifanya katika taifa.
“Lakini Mwalimu alisisitiza kung’atuka na maisha ya Watanzania yakaendeelea na maendeleo yakaendelea kupatikana nchini. Tukikumbuka tukio hilo ndani ya mwaka huu, hilo ni funzo kubwa Mwalimu Nyerere alilotuachia ambalo ni ujasiri wa kustahimili mambo makubwa katika nchi yetu,” alieleza.
UMADHUBUTI WA CCM
Shaka amesema tangu Mwalimu Nyerere alipofariki dunia Oktoba 14, 1999, CCM imeendelea kusimamia umadhubuti wa kuwa chama imara cha siasa katika kuisimamia serikali, kama ambavyo alivyokuwa akisisitiza kwamba bila CCM madhubuti nchi itayumba.
“Umadhubuti wa kwanza ni kushinda dola, hakuna umadhubuti mwingine wa chama cha siasa pale kinapopoteza dola, ukipoteza dola ina maana umepoteza umadhubuti na uimara wako. Kwa hiyo CCM itaendelea kuwa imara kwa sababu imeendelea kushinda na kuongoza kushika dola zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,” amesema.
Amesema mbali na hilo, CCM inaendelea kujivunia umoja na mshikamano ulipo miongoni mwa wananchi.
Shaka alieleza kuwa chama kinaendelea kuimarika siku hadi siku, pamoja na kupita katika dhoruba mbalimbali ya kisiasa ambayo baadhi ya watu walikuwa wakiamini kitasambaratika.
“Umoja na mshikamano wa wana CCM unazidi kuimarika siku hadi siku. CCM imekuwa ikipita katika dhoruba kubwa kiasi kwamba kwa mtu mwepesi anaweza kusema kimepoteza mwelekeo.
Alibainisha kuwa: “Mwaka 2015 hakuna aliyetegemea CCM ingeendelea kubaki kama ilivyo sasa, wengi walijua inakwenda kugawanyika, lakini CCM ikabaki kuwa imara na kushinda dola.”
Alisema hayo ni mafanikio makubwa ambayo chama kinajivunia kwa kubaki kuwa kimoja.
DEMOKRASIA
Akizungumzia namna ambavyo CCM inasimamia misingi ya demokrasia kama ambavyo Mwalimu Nyerere alivyokuwa akisisitiza, Shaka alisema daima CCM ndiyo mama wa demokrasia katika siasa za Afrika.
Alisema katika kuthibitisha hilo, ndani ya chama kuna mfumo mzuri wa viongozi kupokezana madaraka na hata kinapopoteza kiti katika uchaguzi, kimekuwa kikikubali.
“Chama kinaendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kushinda uchaguzi kwa haki na amani. Ndiyo maana katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde, CCM ijitokeza kuwapongeza hadharani wenzetu walioshinda uchaguzi huo.
“Tumefanya hivyo siyo kwa bahati mbaya, kwa sababu tumekubali kuishi katika dhana ya demokrasia ya vyama vingi, na ifike mahali tunaposhindwa tukubali na tukishinda wenzetu wakubali,” alisisitiza.
Alieleza kuwa kama CCM ikishindwa kusimamia dhana ya demokrasia kwa vitendo, nchi inaweza kuyumba.
“Ifahamike kuwa CCM ndiyo imeshika hatima ya nchi, ili tufanye mambo yetu vizuri ni lazima tuheshimu misingi na dhana ya demokrasia ya vyama vingi,” alisema.
MAFANIKIO YA RAIS SAMIA
Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi, alisema katika awamu zote sita za uongozi nchini, serikali zote zimetekeza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa kwa kuhakikisha maendeleo kwa Watanzania yanapatikana.
Alisema katika awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Watanzania wana matarajio makubwa, ambapo kwa mwenendo wa serikali inavyotekeleza majukumu yake kuna uwezekano mkubwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ukafanyika kwa zaidi ya asilimia 100.
“Ni jambo ambalo liko wazi kwa mwenendo ambao Rais Samia amekuja nao, ilani ya uchaguzi ya CCM inakwenda kutekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100,” alisisitiza.
Alieleza kuwa katika maeneo mbalimbali nchini miradi mingi ya maendeleo inayogusa huduma muhimu za kijamii, inatekelezwa kwa kasi kuhakikisha nchi inafunguka zaidi.
Alisema ujenzi wa vituo vya afya, miundombinu ya barabara, maji safi na salama miradi hiyo inafanyika kwa usimamizi madhubuti kuhakikisha wananchi wananufaika nayo.
Shaka aliongeza kuwa katika fedha za mkopo wa masharti nafuu wa sh. trilioni 1.3, ambazo serikali inaenda kujenga madarasa, hospitali, vituo vya afya, ununuzi magari ya wagonjwa, mashine za kisasa za matibabu na kuwezesha kaya masikini, zitakwenda kutatua kwa kiasi kikubwa changamoto za wananchi.
“Mgawanyo wa fedha hizo umegawanyika nchi nzima, kwa maana hiyo, nchi inakwenda kufunguka. Tukifanikiwa vizuri katika mradi huu, wananchi wanakwenda kujikwamua kiuchumi.
“Katika miaka 22 bila ya Mwalimu Nyerere, viongozi wetu wameishi katika yale ambayo mwalimu aliyaamini kwa vitendo, kwani wala rushwa wanachukuliwa hatua,” alieleza.
Shaka alitoa rai kwa wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na kuhimiza umoja na mshikamano ili aendelee kutatua changamoto za wananchi katika sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Na MUSSA YUSUPH, Dodoma