KUTOKANA na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Elias Kwandikwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga, kimesema kitamkumbuka kwa mchango wake wa ujenzi wa Chama na kuchochea maendeleo kwa wakazi wa Jimbo la Ushetu, ambalo alikuwa akiliongoza kama mbunge.
Kauli hiyo imelitolewa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlowa, baada ya kutembelea nyumbani kwa marehemu Kwandikwa, katika Kijiji cha Butibu, akiongozana na Kamati ya Siasa ya Mkoa.
Mabala amesema Kwandikwa, alikuwa kiongozi shupavu na msikivu, alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 2015, ambapo aliaminiwa hadi kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za unaibu waziri na uwaziri.
“Tumepata pigo kumpoteza mwana maendeleo halisi. Jimbo la Ushetu lilikuwa na changamoto nyingi, zikiwemo za barabara, umeme, afya na elimu, lakini ndani ya kipindi kifupi tangu ameingia madarakani, amewaunganisha wananchi wake kwa kuhakikisha anatatua changamoto hizo,”amesema Mabala.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Philemon Sengati, amesema taifa limempoteza kiongozi thabiti, ambaye alikuwa hapendi kujikweza, mwana mapinduzi halisi, anayependa wananchi wake na taifa kusonga mbele katika nyanja za kimaendeleo.
“Kwa kuthamini mchango wa mpendwa wetu Kwandikwa, tumefika nyumbani kwa marehemu kuwapa pole wanafamilia kwa msiba huu mkubwa. Serikali tumeanza kuwasiliana na wenzetu walioko Dar es Salaam, kuhusu utaratibu wa mazishi ya kiongozi wetu,” alisema.
Kwa upande wake, mdogo wa marehemu, Emilly Kwandikwa, alisema familia yao imepokea kwa masikitiko kifo cha kaka yao, kwani alikuwa kiongozi, msimamizi wa familia na ukoo wa Mzee Kwandikwa.
“Kaka yangu alianza kuugua juzi, baada ya kujisikia vibaya akiwa kazini, akapelekwa Hospitali ya Rufaa Muhimbili, kisha kupelekwa katika Hospitali ya Jeshi la Lugalo, tukaambiwa amefariki dunia. Sisi kama wanafamilia, tumeumia sana na pengo la kaka yetu halitazibika haraka,”alisema.
Mkazi wa Kijiji cha Butibu, Magdalena Mamba, alisema watamkumbuka Kwandikwa, kwa kuwa amewasaidia kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya afya, kwa kujenga zahanati ya kijiji hicho.
“Tangu aingie madarakani, tumepata maendeleo kwani alikuwa kiongozi wetu, alikuwa mtu wa watu, alitusaidia wanawake kupata mikopo, ambayo imetusaidia kukuza mitaji yetu katika sekta ya ujasiriamali,” alisema.
Na SALVATORY NTANDU, USHETU