SEKRETARIET ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, imeshiriki kwa mtandao maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).
Maadhimisho hayo yameongozwa na Rais wa China, Xi Jinping, ambapo zaidi ya nchi 50 tofauti zimeshiriki ikiwemo Tanzania ikiwakilishwa na Sekretariet ya CCM, ambayo ilikutana leo, Julai 6, katika Chuo cha Uongozi Kibaha.
Pamoja na mambo mengine,Chongolo ameeleza namna ambavyo CPC kimekuwa na ushirikiano wenye manufaa makubwa kwa CCM, ushirikiano ambao umezaa matunda ya urafiki wa kudumu.
Kadhalika amesema pamoja na urafiki wa vyama hivyo viwili, China na Tanzania zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika mambo mengi ya maendeleo, tangu mwaka 1963 ikiwemo ujenzi wa reli ya TAZARA na Kiwanda cha nguo cha Urafiki.