KAMATI Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar, imepongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu ya kutangaza sekta ya utalii wa Tanzania katika ramani ya dunia pamoja vivutio vyake.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Idara ya Itikadi na Uenezi, Catherine Peter Nao, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kikao cha kamati hiyo kilichoketi chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein.
Alisema chama kimeridhishwa na kazi kubwa ya kutangaza sekta ya utalii kupitia vyanzo mbalimbali vilivyopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Catherine alisema kazi ya kutangaza vivutio vya utalii ilianza kwa upande wa Zanzibar, ambapo Rais Samia alitumia ziara yake kuvitangaza vianzio vyote muhimu ambavyo vinautangaza utalii wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Catherine, hatua hiyo ni nzuri ambayo italiwezesha na kulitangaza jina zuri la Jamhuri ya Muungano Tanzania katika ramani ya dunia na kuwafanya wageni wengi kutembelea nchini.
Alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya kuvutia katika sekta ya utalii ambavyo vinahitaji kufanyiwa kazi na kuona wawekezaji wanawekeza nchini.
”Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Zanzibar, katika kikao chake chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM,Dk.Ali Mohamed Shein kimeridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kulitangaza jina zuri la Tanzania katika ramani ya sekta ya utalii duniani,”alisema.
Aidha, katika kikao hicho wajumbe walielezea kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa za kutia saini jumla ya hoja tisa za Muungano ambazo zilikuwa na changamoto mbalimbali na kuwa kikwazo cha kuzorotesha shughuli za maendeleo na uchumi.
Catherine alisema kilichofanywa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sawa na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ibara 11 3(A) ambayo inasisitiza kuimarishwa kwa muungano kuwa imara kwa maslahi ya wananchi wote.
Alisema ufumbuzi wa hoja tisa za muungano sasa zinakwenda kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo na uchumi na kuleta tija kwa taifa.
”Wajumbe wa Kamati Maalumu ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar wamefurahishwa na juhudi zilizochukuliwa na serikali zote mbili SMT na SMZ katika kuzipatia ufumbuzi changamoto za muungano kwa lengo moja la kuufanya muungano kuwa imara zaidi kwa mslahi ya taifa,”alisema.
Kuhusu uchaguzi mdogo wa ubunge, alisema chama kimejipanga kushiriki katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Konde, baada ya mbunge mteule wa CCM, Sheha Mpemba Faki, kujiuzulu.
”Nataka niwaambie wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kwamba, tutashiriki katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Konde, ambapo kwa sasa tunasubiri baraka kutoka kwa Kamati Kuu ya CCM, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Taifa NEC kutangaza kufanyika kwa uchaguzi huo,”alisema.
Na Khatib Suleiman, Zanzibar