Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Imani Kajula, amesema haikuwa kazi rahisi kumpata Kocha mwenye viwango vya hali ya juu kama Abdelhak Benchikha, ambaye anarithi mikoba kutoka kwa aliyemtangulia Roberto Oliviera ‘Robertinho’.
Benchikha alitangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Simba SC Ijumaa (Novemba 24) na jana Jumatatu (Novemba 27) aliwasili nchini sambamba na wasaidizi wake wawili.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Hoteli ya Serena jana Jumanne (Novemba 28), Kajula amesema: “Leo tunatamatisha shauku iliyokuwepo kwa siku kadhaa. Haikuwa jambo rahisi maana lengo letu kama klabu tulitaka mwalimu ambaye atatupeleka mbali. Kumpata mwalimu mzuri ni mchakato mkubwa sana.”
“Mwalimu Benchikha atakuwepo kwa mkataba wa misimu miwili. Bodi ya Simba, menejimenti ya Simba imempa mwalimu uhuru wa kufanya kazi. Sisi ni moja ya klabu bora Afrika hatuwezi kufanya kazi kwa kumbana.”
“Walimu ambao kocha Benchikha amekuja nao ndio aliochukua nao ubingwa wa Shirikisho Afrika na Super Cup. Kocha Farid amefanya kazi na Benchikha kwa miaka 30 pamoja na kocha Kamal amefanya nae kazi kwa karibu.”
Kocha Benchikha anatarajiwa kuanza kazi ya kukiandaa kikosi chake tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaopigwa Botswana Jumamosi (Desemba 02).