KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameitaka Serikali kuanza ujenzi wa viwanda vya nguo katika Mkoa wa Simiyu na maeneo mengine inakolimwa pamba kwa wingi.
Chongolo ameyasema hayo akiwa katika ziara ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa katika Mkoa wa Simiyu, yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza uhai wa Chama mashinani.
“Ni lazima mtengeneze mazingira ya kuwa na pamba inayoanzia hapa na kuvaliwa hapa. Kiwanda kijengwe hapa Bariadi na pamba ichakatwe hapa ili matokeo yaonekane, lazima tuweke msukumo viwanda vijengwe hapa, na nguo zinazotokana na pamba yetu kwa sababu ni bora na nguo zitakuwa bora,” amesema.
Chongolo ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, akieleza mafanikio wanayotarajia kuyapata katika uzalishaji wa pamba mwaka huu.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu alitembelea na kukagua mashamba ya wakulima wa pamba katika wilaya ya Bariadi, maendeleo ya ujenzi wa ofisi za CCM za matawi na Kata, ujenzi wa barabara ya Somanda – Isakalyamhela na kuhudhuria mkutano wa shina namba 8, Kata ya Nkololo.
Katika ziara hiyo, Chongolo aliambatana na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Simiyu, Shamsa Mohammed Seifu na Mkuu wa Mkoa huo, Kafulila.
Na MWANDISHI WETU



























