WAJUMBE wa Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, wameonya kwamba wao siyo viongozi wa kupiga porojo na hawako tayari kuona Ilani ikihujumiwa.
Katika taarifa yao ya kuhitimisha ziara ya siku mbili mkoani Rukwa, wajumbe hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, wamesema katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2021, hawatamvumilia kiongozi au mtendaji wa serikali ambaye atakuwa kikwazo katika kuitekeleza kwa ufanisi.
Wajumbe wengine ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali mstaafu Lubinga, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Kenani Kihongosi.
Katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa Sumbawanga, mkoani humo juzi, Chongolo alisema ziara yao iliyoanza Jumatano na juzi, kutembelea mashina ya CCM, wameshuhudia miradi ambayo thamani ya fedha hailingani na viwango vya miradi husika.
Chongolo alitoa mfano wa Hospitali za wilaya za Nkasi na Kalambo, kila moja imepatiwa sh. bilioni 2.3 ambapo ujenzi wa miradi hiyo hauridhishi, kwa sababu thamani ya fedha hailingani na kazi iliyofanyika.
Kutokana na hali hiyo, Chongolo, alimuagiza mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti, kuhakikisha ndani ya siku zisizozidi 14 ujenzi wa hospitali hizo unalingana na thamani ya fedha na kwamba maelekezo hayo siyo porojo.
“Tunamaanisha, siyo kurembaremba, ni lazima tufanye kazi yenye tija,” alisema Katibu Mkuu Chongolo katika kikao hicho kilichohudhuriwa na viongozi na watendaji wa CCM, viongozi na watendaji wa serikali, madiwani pamoja na wabunge.
“Wananchi wakiona mambo hayaendi, watatuona sisi tunapiga porojo, na sisi hatuko tayari kuitwa wapiga porojo,” alionya mtendaji mkuu huyo wa CCM.
Kero nyingine ambayo wananchi wanakumbana nayo ni ukosefu wa dawa katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, licha ya serikali kutoa fedha nyingi kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo.
Katibu Mkuu Chongolo alisema atawasiliana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima na uongozi wa Bohari ya Dawa (MSD), kujua mamilioni ya fedha yanayotolewa kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa dawa yanakwama wapi.
“Tunataka watueleze nani anasababisha mkwamo katika upatikanaji wa dawa. Nasema hivi, sisi viongozi tunawajibu wa kufuatilia na kusimamia thamani ya fedha katika kila eneo,” alisema.
Alisema kila kiongozi na mtendaji katika Chama na serikali anawajibu wa kutimiza wajibu wake kwa kuhakikisha upatikanaji wa tija una kuwepo.
“Tutakuwa wakali, ni lazima tuogope fedha ya umma, ukizitumia vizuri zitakujengea heshima, ukizitumia vibaya zitakuvunjia heshima, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mwadilifu,” alisisitiza.
Kuhusu migogoro ya ardhi, Chongolo alimuagiza Mkirikiti na wakuu wa wilaya za mkoa wa Rukwa kutafuta suluhisho la kero hiyo, ambayo imekuwa ikipoteza muda mwingi wa wananchi, ambao wangeutumia katika uzalishaji mali.
Kuhusu maji, Chongolo alisema bado ni changamoto na kudokeza kwamba ni wakati muafaka kuanza kufikiria kuwa na mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Tanganyika kwa ajili ya mkoa wa Rukwa.
Kutokana na wananchi kulalamikia tatizo hilo, alilazimika kuzungumza na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ambaye alimhakikishia kwamba atakwenda mkoani humo kushughulikia tatizo hilo.
“Nadhani ni wakati muafaka, hebu tufikirie kuwa na mradi mmoja mkubwa wa maji katika ziwa Tanganyika kuweza kumaliza changamoto hii kwa muda mrefu,” alisema.
Jana na leo, Katibu Mkuu Chongolo na wajumbe hao wa sekretarieti watakuwa na ziara ya kutembelea mashina ya CCM, katika wilaya za mkoa wa Songwe.
Na MWANDISHI WETU