KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameipongeza Serikali kwa kumaliza adha ya muda mrefu waliyokuwa wakiipata watumiaji wa barabara ya Mpanda (Katavi) – Tabora, baada ya ujenzi wake wa kiwango cha lami kukamilika na kuanza kutumika, katika hatua ya uangalizi.
Akizungumza na wananchi akiwa njiani kwenda Tabora, baada ya kumaliza ziara ya siku mbili Katavi, Chongolo alisema ujenzi na kukamilika kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 335, ambayo ni kiunganishi muhimu cha mikoa hiyo miwili na mingine ya Magharibi mwa nchi, ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.
“Hongereni sana kwa Serikali na TANROADS, kwa maana mmefanya kazi nzuri ya usimamizi, barabara imejengwa kwa kasi, nzuri lakini pia mmesimamia thamani ya fedha vizuri,” alisema.
Chongolo alisema kukamilika barabara hiyo kuanze kutafsiri uchumi wa wananchi wa maeneo hayo kwa sababu fursa nyingi zitafunguka, hivyo ni vyema wakazi wa eneo hilo waanze kunufaika na matunda ya barabara hiyo.
Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa Katavi, Mhandisi Martin Mwakabende, alisema wakati mkoa unaanzishwa ulikuwa na kilomita 1.9 tu za barabara ya kiwango cha lami na mpaka sasa mkoa huo una barabara za lami zenye urefu wa kilomita 322.
“Jumla ya kilomita zinazokwenda kujengwa ni 335, ambazo zimegawanywa katika vipande vitatu, kuna kipande cha kwanza kinaanzia Ususula kuja Komanga kina urefu wa kilomita 108, lakini pia kuna kilomita tisa zimepita kwenye mji wa Sikonge.
“Kipande cha pili kinaanzia Komanga mpaka Kasinde kina kilomita 108, lakini pia kina kilomita 4.2 zimepita katika mji wa Inyonga na cha tatu kinaanzia Kasinde kuja Mpanda kina kilomita 105 na katika mradi huu serikali imewekeza kiasi cha sh. bilioni 432.8,” alisema.
SEKRETARIETI ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapindunzi (CM), ikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, imehitimisha ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na kuimarisha Chama mashinani katika mikoa ya Kagera, Geita, Kigoma, Katavi na Tabora.
Na MWANDISHI WETU, Tabora



























