KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amewaagiza viongozi wa Chama na serikali kuhakikisha wanahamasisha wananchi kuiunga mkono sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchi nzima mwakani.
Chongolo amesema masuala ya sensa yasihusishwe na mambo ya kisiasa kwa sababu mipango ya nchi nyingi duniani inaendana na takwimu ambazo matokeo yake ni kuleta uchumi na maendeleo.
Ametoa maagizo hayo, akiwa ziarani mkoani Lindi, ziara ambayo ameambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
“Viongozi kila mmoja arudi kwenye eneo lake, maandalizi ya zoezi la sensa 2022 yawe sehemu ya mazungumzo yenu kila siku, nendeni mkajiandae sensa ina tija,” amesema.
Katibu mkuu huyo amefafanua kuwa bila takwimu sahihi ya idadi ya watu katika eneo, serikali haiwezi kujua mahitaji ya wakazi wa eneo husika.
Amesema serikali ina utaratibu wa kufanya sensa ya watu kila baada ya miaka 10, lakini baadhi ya watu wanahusisha hatua hiyo na masuala ya kisiasa.
“Watu wengi wanakuja na kuhusisha masuala ya sensa na siasa, sensa katika nchi ndio uchumi na ndio maendeleo..,” alisisitiza.
Kadhalika, alisema watu watakapohamasika na kujitokeza katika zoezi hilo, nchi itakuwa vizuri katika mipango yake na watu wakihesabiwa kwa nidhamu itasaidia kuleta maendeleo katika nchi.
Maagizo hayo ya Chongolo, yamekuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuzindua mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa hiyo.
Katika hafla ya uzinduzi huo, iliyofanyika jijini Dodoma, Rais Samia alisema sensa ni muhimu kwa sababu inakwenda kusaidia utekelezaji wa mipango ya Serikali.
Alisema kwa kutambua idadi ya watu na shughuli wanazozifanya, inasaidia serikali kujipanga vyema katika ugawaji wa rasilimali.
Hata hivyo alisema wapo watu wanaibeza serikali kutumia fedha za ndani ili kufanya sensa hiyo, hoja aliyoijibu kwamba ni muhimu kwa taifa kuwa na takwimu zake.
“Kumekuwa na hoja kwanini Tanzania itumie fedha hizo kwenye zoezi la sensa, sababu ni kwamba kama tunaweza kufanya wenyewe na kupata idadi yetu kwanini tutumie namba zinazotolewa na vyombo vingine vya kimataifa,” alisema.
Rais alisisitiza zoezi hilo lifanywe kwa ufanisi kwa maana ya muda na gharama nafuu, ikizingatiwa nchi bado inapambana kujinasua katika changamoto ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la uviko-19.
Mara ya mwisho, Tanzania ilifanya sensa ya watu na makazi mwaka 2012, ambapo idadi ya watu ilitajwa kuwa milioni 44.9.



























