WACHIMBAJI wadogo wa madini wilayani Shinyanga, wameaswa kuilinda miundombinu ya maji inayoendelea kusambazwa katika maeneo yao ya makazi na kuwataka wasiikate wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo, wakati akikagua ujenzi wa tangi la maji lenye lita za ujazo 500,000 lililojengwa katika Kijiji cha Mwakitolyo,mkoani Shinyanga.
Tanki hilo linajengwa kwa gharama ya sh. milioni 394.13 ambazo ni za serikali na ujenzi wake umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilika mwezi ujao ambao utawanufaisha wananchi zaidi ya 14,600 wa kijiji hicho.
Chongolo alisema mradi huo unatekelezwa na serikali kwa gharama kubwa, hivyo wachimbaji hao ni lazima wailinde miundombinu ya maji na wasikate mabomba ya maji yanayoendelea kusambazwa katika eneo hilo wakati wakifanya uchimbaji wa madini.
“Mradi huu ni fedha za wananchi,serikali inautekeleza kwa gharama kubwa na hapa Mwakitolyo ni kijiji cha wachimbaji madini sasa niwaase msikate mabomba ya maji katika shughuli zenu za uchimbaji,mkiharibu miundombinu hii mnaharibu fedha za maendeleo kwa wananchi,”alisema.
Aliwataka wachimbaji hao wadogo kutumia fursa waliyopewa na serikali ya kutenga maeneo ya wachimbaji wadogo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji ili nao wapate fedha na kuinua uchumi wao.
“Serikali inawapenda imewatengea maeneo ya uchimbaji mdogo na inawaletea miradi ya maendeleo kama hii ya maji sasa niwatake tumieni fursa hii vizuri, fedha mnazopata zitumieni kuleta maendeleo yenu na sio kuzitapanya,”alisema.
Awali, akitoa taarifa ya mradi huo wa tangi la maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Kahama Shinyanga (KASHWASA),Patrick Nzamba, alisema mradi huo utakamilika Juni 2,mwaka huu.
Patrick alisema mradi huo umetekelezwa kwa awamu tatu na kwa sasa awamu mbili za mradi ujenzi wake umefikia asilimia 98 na awamu ya tatu itakuwa ni usambazaji wa maji utakaotumia shilingi milioni 615.3.
“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa tangi umekamilika kwa asilimia 98 ,pia ujenzi wa uzio nao uko asilimia 90 awamu ya tatu ni Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Shinyangay(RUWASA), wataanza kazi Julai mosi, mwaka huu,”alisema.
Awataka wananchi kuchangamkia zao la Tumbaku
Chongolo akiwa wilayani Kahama, mkoani hapa aliwataka wananchi wa mkoa huo na maeneo mengine kuchangamkia kilimo cha tumbaku kwa kuwa tayari serikali ya CCM imeshughulikia changamoto ya bei.
“NimezungumzanaWaziriwaKilimo, Hussein Bashe, kuhusu mpango wa wakulima, ameniambia kuwa mpango ni kuzalisha tani 100,000 au kilogramu milioni 100 za mazao haya, maana yake ninyi wakulima muende kulima maeneo makubwa na kilimo kikubwa ili uzalishaji uanze kupanda kuanzia sasa,”alisema.
Chongolo alisema mnunuzi mkubwa wa zao hilo la tumbaku mkoani Morogoro, alikuwa na changamoto lakini hadi sasa changamoto hizo tayari zimetatuliwa na hivi karibuni Kiwanda hicho kitawashwa kwa ajili ya kufanya uzalishaji, ambapo kiwanda hicho kinahitaji kilo milioni 30, hivyo wakulima wanapaswa kuchangamkia fursa kulima zaidi.
“Tumbaku inauzwa kwa dola 1.65 ipo hapa inauzwa kwa madaraja ukiitunza vizuri zaidi inakwenda hadi daraja la juu inauzwa Shilingi 5000 kwa kilo, sawa na Dola mbili na zaidi, zao la pamba nalo limeni kwa kiwango kikubwa kwa sababu Soko lipo,”alisema





























