NA ESTA MALIBICHE, IRINGA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amewataka vijana walioaminiwa nafasi za uongozi kufanya kazi kwa weledi, ili kundi hilo liendelee kuaminiwa.
Chongolo aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya wenyeviti wa wilaya kutoka Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) nchini, yanayofanyika Chuo cha Mafunzo ya Itikati na Uenezi Ihemi, mkoani humo.
Alisema ipo changamoto kwa vijana wengi waliopewa nafasi za uongozi kushindwa kuzitumikia ipasavyo na kusababisha kuvunja imani kwa mamlaka za teuzi.
Katibu Mkuu huyo wa CCM, aliwasihi wenyeviti wa wilaya wa UVCCM kutumia mitandao ya kijamii vizuri na siyo kuvuruga amani kwa kutoa siri za vikao vya Chama.
Aliwataka viongozi hao, matumizi ya mitandao ya kijamii na umuhimu wa utunzaji wa siri za ndani ikawe ni ajenda muhimu, ingawa wengine wanahuruka zao ambazo zinahitaji siyo tu mafunzo hayo, bali upendo binafsi na kujitambua.
“Katika eneo la mitandao ya jamii na utunzaji wa siri limejaa changamoto nyingi kwenu vijana na inakigharimu sana Chama. Wapo baadhi ya vijana wanaona ufahari kuweka taarifa za Chama zinazotokana na vikao katika mitandao ya kijamii bila ya hata kuruhusiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Napenda kusisitiza siri za Chama ni nyingi siyo za kikao tu, hivyo katika hili wanahitajika viongozi wenye maadili kuhakikisha mambo ya siri ya Chama yanabaki kuwa ya kwetu.”
Chongolo alisema mitandao ya kijamii siyo kwamba haifai isipokuwa anataka kuona inatumika katika kukijenga Chama, badala ya kusababisha migawanyiko na kuleta makundi.
“Kila mmoja wetu katika mafunzo haya awe makini kuwasikiliza watoa mada na kuuliza jambo kama hajaelewa ili akitoka hapa awe ameiva kwa kiwango cha hali ya juu,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Raymond Mangwala ambaye juzi jioni aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, alisema vijana wanapaswa kulinda na kujenga ujamaa na kujipanga kwa hoja sio matusi na viroja mtandaoni.
“Vijana ndiyo taifa la kesho, tunawahitaji na mafunzo haya yakawe chachu kwenu kutumia fursa zinazopatikana na siyo kubishana mtandaoni bila hoja na kujadili mambo binafsi ya watu, badala yake mjikite katika kujadili maendeleo ya umma,”alisema
Naye, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Iringa, Dk. Abel Nyamahanga, alisema lazima vijana wawe na umoja, usawa na mafunzo nia ya kuweka mafunzo haya ni kuendelea kukipa nguvu chama.
“Chama kinatakiwe kiwe na nguvu wakati wote sio nyakati za uchaguzi tu,kwani viongozi wakipewa mafunzo wanakumbushwa kurudi katika maadili ya uongozi,na kuleta mapinduzi ya kimaendeleo kwa jamii na chama,” alisema



























