KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amewaagiza wabunge wa CCM kufanya ziara katika majimbo yao kueleza mambo muhimu yaliyojadiliwa na kupitishwa katika vikao vya Bunge la Bajeti, ambayo yatakwenda kutatua changamoto za wananchi.
Amewataka viongozi wa CCM ngazi za mikoa, wilaya na kata kwenda katika mashina na matawi ya wanachama kufanya mikutano, ikiwemo kuwasikiliza na kutoa mwongozo wa CCM katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025.
Chongolo alisema hayo katika kikao cha ndani na viongozi wa CCM akiambatana na viongozi wa sekretarieti ya CCM ngazi ya taifa , katika mji mdogo wa Laela.
Alisema wabunge wanapaswa kuwaeleza wananchi yale yaliyojadiliwa na bungeni na kupokea maoni yao kwa ajili ya kuyawasilisha bungeni katika vikao vijavyo.
“Nawapongeza wabunge niliowakuta katika mikoa yao, baada ya Bunge la bajeti kumalizika, sasa kazi yenu ni kupita majimboni kuwaeleza wananchi yaliyopitishwa ndani ya bajeti ambayo yanayowagusa.
“Wabunge kaeni kwanza na madiwani, muwasikilize ndipo mpange ratiba ya ziara zenu kwenda kwa wananchi,” alisema Chongolo.
Katibu Mkuu huyo alisema baada ya wabunge kulalamika kuhusu bajeti ndogo ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA), Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kusikia kilio hicho ametoka sh. milioni 500 kwa kila jimbo kwa ajili ya kuimarisha barabara za vijijini na mijini zinazohudumiwa na TARURA.
“Natoa maagizo kwa wabunge wote nchini ambao ni zao la CCM, wamemaliza bajeti,wote waende katika majimbo yao wakawaeleze wananchi yaliyomo katika bajeti yanayowagusa ili waelewe nini serikali inataka kufanya kwao,”alisema.
Katika hatua nyingine, Chongolo akizungumzia uchaguzi ndani ya CCM unaotarajiwa kuanza kufanyika mwakani, alipiga marufuku kupanga safu za uongozi kwa lengo la kujipatia nafasi.
“Hivi sasa kuna watu wameanza kujiandaa kupanga safu za uongozi katika uchaguzi ujao ndani ya CCM, najua na yapo yaacheni hayo yote ni matatizo ndiyo maana lugha ni moja tu tuvunje makundi,” alisisitiza.
Na WILBROAD SUMIA, Rukwa