KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amewataka wana CCM kuhudhuria vikao vya mashina ukiwa ndiyo msingi wa uimara wa Chama.
Akizungumza katika ziara yake na Sekretarieti ya CCM Taifa, mkoani Mbeya, Chongolo amesema kila mwanachama anapaswa kuwajibika katika shina lake.
“Tumekuja huku chini katika mashina kwa sababu huku ndipo ulipo uhai wa CCM, tunazungumza na wanachama wote na ndipo penye wananchi na kwamba kila mwanachama anatoka katika shina,” amesema Chongolo.
Chongolo amefafanua kuwa maendeleo ya wananchi yanatokana na ushirikiano imara kati ya Chama na serikali, hivyo uhusiano huo unapaswa kudumishwa.
“Ni lazima sisi viongozi na watendaji wa Chama na serikali, tuwe na uwezo wa kutenganisha masuala binafsi na kazi tunazowajibika nazo, tukiwa na nidhamu katika hayo na kuyapa kila jambo muda wake nawahakikishia changamoto ya mahusiano, migogoro, ugomvi, kutoelewana, kukunjiana sura kuchukiana, havitakuwa na nafasi,” alisisitiza.
Katika ziara yake hiyo wilayani Kyela, alitembelea shina namba 01 Tawi la Lema, shina namba 01 Tawi la Fubu, shina namba 02 Tawi la Njisi, shina namba 02 tawi la Nazaleth na kusisitiza umuhimu wa mikutano ya ngazi hizo.
“Tumekuja kuhimiza vikao hivi vya Mashina, kwetu sisi vikao hivi ni muhimu kuliko vikao vyote, kwa kiongozi yeyote mwakani anayetaka kugombea uongozi ndani ya Chama lazima awe na muhtasari wa mahudhurio ya vikao vya mashina,” amesema.
Amebainisha kuwa, msingi wa kutoyumba kwa chama unatokana na wanachama kuheshimu uongozi kuanzia ngazi ya shina na kushiriki vikao.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule ya sekondari ya upili (High School) ya Lema, ujenzi wa Kituo cha Huduma ya pamoja Mpakani katika eneo la Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi.
Chongolo na Sekratarieti yake, bado wanaendelea na ziara katika mashina mbalimbali nchini.
Na MWANDISHI WETU