WANANCHI wameaswa kutovaa miwani ya macho, kabla ya kupimwa ili kuepuka madhara makubwa ya kiafya.
Pia, wameshauriwa kuacha tabia ya kununua dawa za macho katika maduka ya dawa, bila kupata maelekezo ya madakatari, kwa kuwa zinachangia kuathiri zaidi macho.
Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mratibu wa Huduma za Macho wa Mkoa wa Pwani, Dk. Elgreta Mzava, alipozungumza na UHURU.
Dk. Elgreta alisema tabia ya watu kununua miwani za macho mitaani bila kupima matatizo waliyonayo na kuelekezwa inayofaa na watalaamu, imechangia kwa kiwango kikubwa kupata madhara makubwa.
Amesema katika Hospitali ya Tumbi, walibaini magonjwa 10 wa macho yanayojirudia hususan mtoto wa jicho. “
Tatizo la mtoto wa jicho likigundulika mapema huwa linatibika na mgonjwa anapona kabisa,” alieleza.
Alitaja changamoto nyingine ya macho ni ukoma au shinikizo la macho ambayo ni vizuri igundulike mapema na kutibiwa kwa sababu wapo wenye tatizo hilo lakini hawatambui kwa sababu ni ugonjwa ambao mtu haumwi.
“Wagonjwa wengi wanaokuja kutibiwa wanakuwa na tatizo hili likiwa hatua za mwisho yaani mbaya zaidi,” alieleza.
Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo la ukoma wa macho, wanajitahidi kutumia huduma za mkoba kwenda vijijini kutoa matibabu na huduma mbalimbali za macho.
“Pia tunapata magonjwa ya maambukizi ya macho, vidonda na watu walioumia macho kutokana na ajali,” alisema na kuwasihi wananchi kutonunua miwani za macho ambazo zinauzwa mitani bila ya kupimwa.
“Mtu akiona ana tatizo la kushindwa kuona maandishi anaenda mtaani kununua miwani ya kusomea bila kupimwa. Miwani ni tiba kama zilivyo zingine, tunashauri waende hospitali na watibiwe,” alisema.
Alitoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kupima macho ili kugundua mapema matatizo waliyonayo.
Na CHRISTOPHER LISSA