KUKOSEKANA elimu sahihi ya afya ya uzazi na matumizi ya dawa za mitishamba za kuongeza uchungu kwa wajawazito mkoani Shinyanga, zimetajwa kuchangia vifo, ambapo kwa mwaka 2021 wajawazito 50 na watoto wachanga 600 walifariki dunia.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Nuru Mkuya, wakati akisoma taarifa ya tathinini ya hali ya vifo vya wajawazito na watoto kwa kipindi cha mwaka 2021 katika mkutano wa wadau wa sekta ya afya.
Amesema takwimu za vifo mwaka 2021 zinaonyesha wajawazito 50 na watoto wachanga 600 walipoteza maisha kutokana na matatizo ya uzazi, ikilinganishwa na mwaka 2020, ambapo vifo kwa wajawazito vilikuwa 46 na watoto wachanga 665.
“Tumejipanga kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii ili ione umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma na kuachana na matumizi ya dawa za mitishamba ambazo zinawaletea madhara,” alisema Mkuya.
Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga, Joyce Kondoro, alisema wajawazito kutumia dawa za kuongeza uchungu kabla ya kujifungua wanajisababishia madhara, kwani wengi wao hupoteza maisha kabla ya kujifungua.
“Tumekuwa tukiwakamata wajawazito wakiwa na dawa za mitishamba ambazo huzimeza ili kuongeza uchungu wajifungue haraka, dawa hizi husababisha kupasuka kwa mfuko wa uzazi na kusababisha mama na mtoto kufariki dunia,” alisema Kondoro.
Mkazi wa Mtaa wa Malunga, wilayani Kahama, Flora Kileo, alisema serikali inapaswa kuwachukulia hatua za kisheria wakunga wa jadi ambao bado wanaendelea kutoa huduma kwa wajawazito, hususani katika maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga, akimwakilisha mkuu wa mkoa huo, Sophia Mjema, aliwataka watumishi wa sekta ya afya kufanya kazi zao kwa weledi kupunguza vifo hivyo.
SALVATORY NTANDU, KAHAMA



























