MKUU wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Khadija Nassir Ally, ameagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kutotoa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali visivyopata elimu ya ujasiriamali.
Khadija aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Wanawake Wilaya ya Mkuranga lililoandaliwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake kuwawezesha kiuchumi ngazi ya mkoa, Mariam Ulega.
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Halmashuri ya Wilaya ya Mkuranga ilitoa mikopo kwa akinamama, vijana na wenye ulemavu, sh. milioni 322 lakini fedha hizo hazijaleta matokeo chanya.
“Hata nikiuliza fedha hizo tulizifanyia nini, najua hakuna atakaye kuwa na majibu sahihi ya alichofanyia.
“Vikundi vilivyoaminiwa kupewa mkopo je vipo tayari kufanya kazi ya kubadilisha maisha yao, jibu ninalopata havipo tayari kwa hiyo Halmashauri ya Mkuranga kupitia Ofisa Maendeleo ya jamii, tusitoe mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali ambavyo havijapewa elimu ya kutosha,” alieleza.
Aliongeza kuwa: “Tusitoe mkopo kwa akinamama, vijana na wenye ulemavu kabla hatujajiridhisha kwamba mkopo huo hautakuwa mzigo kwao bali uwe ni faraja. Nasema hivyo kwa sababu kuna vikundi vinataka kupewa mkopo lakini bado havijajiandaa kujua biashara wanayotaka kuifanya.”
Naye, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu, alikabidhi kuku 2,600 kwa Mwenyekiti wa jukwaa la akinamama Mkoa wa Pwani ambaye naye alikabidhi kuku hao katika vikundi 17 vya wanawake.
Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Mariam Ulega aliwataka akinamama hao kufuga kuku hao kwa umakini kwa lengo la kutosheleza soko la kuku la wilayani humo na hata kupeleka katika Jiji la Dar es Saalaam.
“Tunataka kuku sasa watoke Mkuranga na sio mkoani Singida, hivyo kila mmoja akafuge kuku kwa umakini mkubwa ili kupata tija,” alieleza.
Na Scolastica Msewa, Mkuranga



























