Na MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kwa kuunda kamati za kushughulikia malalamiko wakati wa utekelezaji wa miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kuanzia ngazi ya Mtaa hadi Wilaya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo na mwongozo wa kushughulikia malalamiko hayo Wilayani Kinondoni, Gondwe ametoa maagizo kwa kamati hizo kuleta mrejesho wa malalamiko yaliyopokelewa na yaliyoshughulikiwa kwa wakati ili ufanisi wa kamati hizo uonekane.
“Nimefurahi kuona DAWASA wamefika hadi Kinondoni kutatua kero za wananchi kwa kasi, hivyo nipende kuzikumbusha hizi kamati za mitaa hadi wilaya zilizoundwa zikatimize majukumu yake kwa kutatua kero zitakazoibuliwa kwa wakati” amesema Gondwe.
Akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Sipora Liana, amesema utatuzi wa kero za wananchi katika kila sekta hususani wakati wa utekelezaji wa miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, ni maelekezo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye ameagiza kero na malalamiko ya wananchi yasisubiri viongozi wa kitaifa zitatuliwe katika ngazi za chini.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Mhandisi Modester Mushi, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, ameishukuru Wilaya ya Kinondoni kupitia Mkuu wa Wilaya kwa kutoa nafasi ya kuundwa kwa kamati hizo.
Mhandisi Modest amesema mafunzo ya kusimamia malalamiko kwenye miradi ya majisafi imekwishafanyika katika wilaya za Ubungo, Ilala, Kigamboni, Kinondoni na Kibaha Mkoani Pwani.



























