JESHI la Polisi limethibitisha kuwa, Hamza Mohammed aliyeuawa wiki iliyopita alikuwa gaidi wa kujitoa mhanga aliyekuwa akijifunza vitendo hivyo kupitia mitandao ya kijamii inayomilikiwa na makundi ya ugaidi duniani likiwemo la Al Shabab.
Hamza aliuawa Agosti 25, 2021 baada ya kutekeleza mauaji ya askari wanne, watatu kati yao wa polisi na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi ya SGA kwa risasi jirani na balozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura, akizungumza jijini Mwanza na waandishi wa habari amesema katika uchunguzi waliofanya wamebaini kijana huyo alikuwa na viasharia vyote vya ugaidi kwa muda mrefu.
“Hamza Mohammed ni mtu ambaye alikuwa akiishi kisiri na mtu aliyegubikwa na viashiria vyote vya kigaidi kipindi cha kutosha.
Hamza amekuwa akijifunza mambo mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii ambayo kwa kipindi kirefu amekuwa akijifunza mambo ya kigaidi kupitia mitandao inayoonyesha matendo ya Al Shabab na matendo ya vikundi kama ISIS yanayoendelea na magaidi wengi hujifunza kupitia mitandaoni,” amesema Wambura.
Amesema uchunguzi wao ulijikita katika mambo makuu matatu: kutaka kutambua Hamza Mohammed ni nani, nini kilimsukuma kwenda kufanya tukio lile na kutaka kutambua mshiriki mwingine katika tukio hilo.
“Tabia zake na matendo yake kwa kipindi kirefu ameyapata kupitia mawasiliano na watu wengine wa baadhi ya nchi ambazo zina matendo kama hayo lakini kikubwa ni ugaidi kupitia mitandao yaani radicalisation (misimamo mikali) kupitia social media (mitandao ya kijamii),” amesema Wambura.
Amebainisha kuwa, katika kuthibitisha kuwa Hamza alikuwa gaidi kutokana video zilizosambaa mtandaoni alikuwa anashambulia gari la polisi bila uwoga na hiyo ni kudhihirisha kuwa alikuwa haogopi na nia yake ni kuua askari.
Hata hivyo, amekanusha madai kuwa aliwashambulia askari hao kwa sababu walimdhulumu madini yake ambapo amesema katika uchunguzi wao wamebaini kuwa kijana huyo hakuwa madini wala fedha.
“…watu wengi wameongea kwamba alikuwa anamiliki migodi ya madini kule Chunya na maeneo ya Makongolosi uchunguzi wetu umebaini hali hiyo ya maisha ilikwisha simama muda mrefu,” amebainisha Wambura.
Aidha, Jeshi la Polisi lamebaini kuwa, Hamza alikuwa kwenye kundi la magaidi wanaoamua kuifia dini.
Wambura amewahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi limejitoa mhanga kuhakikisha linalinda raia na mali zake ili iwe salama kama walivyofanya kwenye tukio la Hamza.
Na Johari Shani, Mwanza



























