Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo ( Mb) ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) kwa kazi nzuri yenye ufanisi mkubwa katika kuhudumia shehena inayopita katika Bandari ya Dar es Salaam, hali inayorahisisha ufanyaji biashara nchini.
Dk. Jafo ametoa pongezi hizo Septemba 9,2024 alipotembelea na kukagua shughuli za utekelezaji Bandarini hususani katika kituo cha mita za kushushia mafuta ( flow meter) cha Kurasini Oil Jet ( KOJ) kilichopo Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema ufanisi katika kuhudumia Shehena mbalimbali ikiwemo Shehena ya mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam kunachangiwa zaidi na uwekezaji uliofanyika katika Bandari hiyo ambao umeleta tija na ufanisi zaidi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abeid Galus amesema ufanisi unaonekana sasa katika Bandari ya Dar es Salaam unachangiwa na uwekezaji Mkubwa wa Miundombinu na Vifaa vya Kisasa uliofanywa na Serikali ambapo Meli sasa inatumia siku tatu hadi nne kuhudumiwa kutoka siku saba za awali.
Amesema pia idadi ya siku za Meli kusubiri kuingia Bandarini ili kuhudumiwa gatini zimepungua kutoka siku 30 za awali hadi siku siku tano hadi saba pekee na hivyo kuongeza ufanisi katika kuhudumia shehena Bandarini.