WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, amewaelekeza wazalishaji, wasambazaji na wafanyabishara wa vifaa vya ujenzi na vinywaji baridi kushusha mara moja bei za bidhaa hizo walizopandisha kiholela na kuuza bidhaa hizo kwa kuzingatia gharama halisi za uzalishaji na usambazaji.
Kauli hiyo ameitoa leo Februari 7, 2022, jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Wizara kuhusu mwenendo wa uzalishaji na usambazaji wa vifaa vya ujenzi katika kipindi cha mwezi Novemba 2021 hadi mwezi Februari 2022.
Agizo lingine amezielekeza Mamlaka zote za udhibiti kuchukua hatua kali dhidi ya walimbikizaji na wauzaji kupitia mlango wa nyuma (black market) wanaosababisha bei za bidhaa kupanda sokoni, ili kuhakikisha kuwa bidhaa zinafika sokoni kwa wakati na kwa bei shindani.
Aidha, amesema kwa kuwa kitendo cha kupanga bei kati ya washindani ni uhujumu uchumi, ninazielekeza Mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kupanga bei kwa bidhaa kwa mujibu wa sheria za Nchi.
“Ninawaelekeza wazalishaji kuzalisha bidhaa hizo kulingana na uwezo wa viwanda uliosimikwa ili kukidhi mahitaji ya soko, Pia wazalishaji wa vifaa vya ujenzi kuweka mifumo mizuri ya usambazaji wa vifaa hivyo ili kuzuia kupanda kwa bei kunakoweza kuzuilika,”amesema.
Vilevile, amewaelekeza Maafisa Biashara wa Mikoa kote nchini waendelee kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye maeneo yao na kuwasilisha taarifa hizo mara kwa mara Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, kupitia Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, ili itakapobidi hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
NA SELINA MATHEW, DODOMA



























