RAIS Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amewataka vijana kuishi katika falsafa ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere ya kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa bidii na kuepuka ukabila.
Pia, katika kumuenzi Mwalimu Nyerere, amewataka vijana wafanye kazi kwa bidii ili kulifikisha taifa katika uchumi mzuri.
Dk. Kikwete amesema hayo Dar es Salaam, wakati akifungua kongamano la 13 la kusherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema ili taifa lifi ke mbali zaidi, linahitaji vijana wenye uzalendo na wenye uchungu wa nchi yao katika masuala ya maendeleo.
“Vijana ni lazima wawe na uchungu na nchi yao bila kuangalia ukabila na udini kwani wakifanya hivyo, watakuwa wamerithi falsafa za Baba wa Taifa,” alisema
Dk. Kikwete. Dk. Kikwete alisema Watanzania wanaposherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere ni lazima waishi kwa falsafa zake ili nchi iendelee kuwa na amani, mshikamano na umoja.
“Taifa linaweza kufi ka mbali zaidi katika uchumi wake ikiwa vijana watafuata falsafa zilizoachwa na Mwaliu Nyerere ambazo zinaelezea mshikamano wa kweli katika kuleta maendeleo,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Willium Anangisye, alisema baada ya kongamano hilo la siku tatu kumalizika, watamuenzi Mwalimu Nyerere kwa namna yao.
Alisema mambo yote yaliyozungumzwa, yatawekwa katika chapisho moja ili kumuenzi na kumkumbuka hayati Mwalimu Nyerere.
“Sisi chuo kikuu tutamkumbuka Mwalimu Nyerere kwa kuandaa chapisho maalumu linaloongelea falsafa za Mwalimu Nyerere lengo likiwa kumuenzi katika uzalendo wake,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Hakielimu, Dk. John Kilago, alisema katika miaka 100 ya Mwalimu Nyerere kuna mambo mengi ya kuyaenzi ikiwemo uelimishaji.
Alisema katika suala la uelimishaji, inatakiwa vijana kuwapatia elimu na ujuzi ili waweze kusonga mbele katika kuiletea nchi maendeleo.
“Tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuwapatia vijana elimu bora na ujuzimzuri ili waweze kufaidika na rasilimali za nchi,” alisema Dk. Kilago.
Na REHEMA MAIGALA