KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji Tanzania, Dk. Anna Makakala, amesema kazi ya kuwasaka wahamiaji haramu inaendelea kufanyika nchi nzima na mafanikio makubwa yamepatikana.
Amesema hayo wakati akihojiwa na UHURU katika Ofisi za Jeshi hilo zilizopo Kurasini, Jijini Dar es Salaam.
“Kazi hii inaendelea kufanyika, ndiyo maana kila kukicha unasikia wahamiaji haramu wanakamatwa, wanafikishwa mahakamani wengine wamefungwa. Wengine wamelipa faini, wengine wamerudishwa katika nchi zao,” amesema.
Amesema kazi hiyo imekuwa ikifanyika kwa umakini wakishirikiana naa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini, viongozi wa mikoa, wilaya, kata na vijiji ili kuwanasa watu hao wanaoishi nchini kinyume cha sheria.
Amesema kwamba, kutokana na hali hiyo, mirahaba ya serikali imeongezeka kutokana na wageni wengi kufuata sheria za nchi.
UTOAJI VIZA
Kuhusu utoaji viza Dk. Makakala amesema; “Kuanzia Machi mwaka jana hadi sasa karibu viza 400,000 zimetolewa kwa wageni walioomba kuja nchini kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwekezaji.”
Hata hivyo, Dk. Makakala ameeleza mafanikio ya kuwakamata wageni haramu zaidi ya 22,834 ambao waliingia nchini kinyume cha sheria na kuchukuliwa hatua.
Dk. Makakala amewaomba wananchi watoe taarifa katika ofisi za Uhamiaji zilizopo sehemu mbalimbali nchini, kama watabaini kuwepo watu kutoka nje ya nchi wasiowafahamu.
“Ni vyema wakafanya hivyo ili wanaowahifadhi wageni wakamatwe, wananchi wanaofanya hivyo ni vyema wakaacha kwani mtu akikamatwa amehifadhi wageni, atakumbana na adhabu kali kama kufungwa, kutaifishwa mali zake au kukabiliwa na adhabu zote mbili,” amesema.
USAHILI
Akizungumzia kuhusu usahili wa vijana 820 waliopelekwa kambini hivi karibuni baada ya kufuzu vigezo, Dk. Makakala amesema vijana hao, wanaendelea na mafunzo ya kijeshi baada ya taratibu zote za kuwapa kutimizwa kwa mujibu wa sheria.
“Usahili wa vijana wale ulifanyika kwa umakini mkubwa, ili kuwapata watu wenye vigezo sahihi, nashukuru Mungu tumewapa na sasa wapo kambini kwa ajili ya mafunzo,” amesema.
Hata hivyo, Dk. Makakala amesema kwamba, lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuwa na askari wenye weledi.
PONGEZI KWA RAIS SAMIA
Dk. Makakala amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia Serikali kutoa fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za jeshi hilo.
“Tunamshukuru Rais kwa kutupa fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali zikiwemo za ujenzi wa miradi mbalimbali kama vile Makao Makuu ya Jeshi la Uhamiaji huko Dodoma, kulipa madeni, stahiki ya askari na mambo mengine,” amesema.
Pia, amewashukuru watendaji wa jeshi hilo, wakiwemo askari kufuatia kufanya kazi kwa ushirikiano.
“Kazi hii, imekuwa inafanyika kwa ushirikiano mkubwa ndani ya jeshi hili, hakika ninawashukuru watendaji wote, askari na wadau wetu kwa kutupa ushirikiana mkubwa,” amesema Dk. Makakala.
Na ATHANAS KAZIGE



























