HALI ya kuelewana kwa baadhi ya watendaji wakuu serikalini hususan mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu wao, imeonekana kuwa na walakini, hivyo kuwaweka viongozi hao katika hatari ya kuwajibishwa na mamlaka za uteuzi.
Uhalisia huo umebainika, baada ya Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, kueleza jinsi ambavyo yeye na Rais Samia bado hawajaridhishwa na hali iliyopo miongoni mwa wateule wao wizarani.
Dk. Mpango alitoa maelezo hayo wakati akiwasilisha salamu zake kwa umma, katika hafla ya uapisho wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Naibu wake, Pauline Gekul, Naibu Waziri wa Habari, Kundo Mathew na wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika hafla hiyo, Dk. Mpango, alisema amepokea taarifa kutoka baadhi ya wizara, zikionyesha kuwa, bado maelekezo yao kuhusu umuhimu wa umoja na ushirikiano baina ya watendaji wakuu wizarani, hayatekelezwi.
“Mheshimiwa Rais kwa taarifa zinazonifikia, katika baadhi ya wizara, bado somo la kufanya kazi kwa pamoja kati ya mawaziri na naibu mawaziri, katibu wakuu na naibu makatibu wakuu, hili somo nadhani bado halijazama vichwani.
“Kwa hiyo, nipende kuwakumbusha tena, Mheshimiwa Rais alishasema hapa, yeye hana hulka ya kuanza kukaripia watu wazima hadharani, lakini aliwaambieni kwamba anapenda zaidi kuzungumza na kalamu kwahiyo nawasihi mchukulie maneno haya kama ni onyo kutoka kwa msaidizi mkuu wa Rais juu ya haya ambayo tunayaona,” alisema.
Makamu huyo wa Rais alisisitiza, mtu akiwa kiongozi anatakiwa ajitahidi kuwa mnyenyekevu katika kazi yake, kwa kuwa ameteuliwa na kupewa dhamana na Rais, kwa sababu ambazo Rais mwenyewe anazifahamu, hivyo hakuna sababu ya mtu kuinua mabega na kujisikia.
Alitumia nafasi hiyo kuwasihi viongozi wakuu wa wizara ya utamaduni, kujituma kwa uwezo wao wote ili kuisaidia serikali kuwa na uchumi thabiti kupitia sekta za michezo, sanaa na utamaduni alizozitaja kuwa na mchango mkubwa zikisimamiwa vizuri.
Septemba 13, mwaka huu, jijini Dodoma, Rais Samia alitumia hotuba yake ya uapisho wa viongozi aliowateua, akiwemo Waziri wa sasa wa Ulinzi, Dk. Stergomena Tax, kuwafunda viongozi serikalini juu ya masuala mbalimbali likiwemo la kuheshimiana na kushirikiana katika utendaji wa majukumu yao.
Na WILLIAM SHECHAMBO





























